← Hosea (6/14) → |
1. | Njoni, tumrudie Bwana; maana yeye amerarua, na yeye atatuponya; yeye amepiga, na yeye atatufunga jeraha zetu. |
2. | Baada ya siku mbili atatufufua; siku ya tatu atatuinua, nasi tutaishi mbele zake. |
3. | Nasi na tujue, naam, tukaendelee kumjua Bwana; kutokea kwake ni yakini kama asubuhi; naye atatujilia kama mvua, kama mvua ya vuli iinyweshayo nchi. |
4. | Ee Efraimu, nikutendee nini? Ee Yuda, nikutendee nini? Kwa maana fadhili zenu ni kama wingu la asubuhi na kama umande utowekao mapema. |
5. | Kwa sababu hiyo nimewakata-kata kwa vinywa vya manabii; nimewaua kwa maneno ya kinywa changu; na hukumu yangu itatokea kama mwanga. |
6. | Maana nataka fadhili wala si sadaka; na kumjua Mungu kuliko sadaka za kuteketezwa. |
7. | Lakini wao wamelivunja hilo agano kama Adamu; huko wamenitenda mambo ya hiana. |
8. | Gileadi ni mji wa hao watendao maovu, umetiwa rangi ya damu. |
9. | Na kama vile makundi ya wanyang'anyi wamwoteavyo mtu, ndivyo kundi la makuhani wauavyo katika njia ielekeayo Shekemu; naam, wametenda mambo maovu sana. |
10. | Katika nyumba ya Israeli nimeona jambo bovu kabisa; huko uzinzi umeonekana katika Efraimu; Israeli ametiwa unajisi. |
11. | Tena, Ee Yuda, wewe umeandikiwa mavuno, hapo nitakapowarudisha wafungwa wa watu wangu. |
← Hosea (6/14) → |