← Hosea (5/14) → |
1. | Sikieni haya, enyi makuhani, sikilizeni, enyi nyumba ya Israeli, tegeni masikio yenu, enyi wa nyumba ya mfalme, kwa kuwa hukumu hii yawahusu ninyi; maana mmekuwa mtego huko Mizpa, na wavu uliotandwa juu ya Tabori. |
2. | Nao walioasi wameongeza sana ufisadi wao; lakini mimi ndiye awakaripiaye wote pia. |
3. | Mimi namjua Efraimu, wala Israeli hakufichwa nisimwone; maana sasa, Ee Efraimu, umefanya uzinzi; Israeli ametiwa unajisi. |
4. | Matendo yao hayatawaacha kumgeukia Mungu wao; maana roho ya uzinzi imo ndani yao, wala hawamjui Bwana. |
5. | Na kiburi cha Israeli chamshuhudia mbele ya uso wake; kwa sababu hiyo, Israeli na Efraimu watajikwaa katika uovu wao. Yuda naye atajikwaa pamoja nao. |
6. | Watakwenda na makundi yao ya kondoo na ng'ombe wamtafute Bwana; lakini hawatamwona; amejitenga nao. |
7. | Wametenda kwa hila juu ya Bwana; maana wamezaa wana wageni; sasa mwezi huu uandamao utawala pamoja na mashamba yao. |
8. | Pigeni tarumbeta katika Gibea, na baragumu katika Rama; pazeni sauti ya hofu katika Beth-Aveni; nyuma yako, Ee Benyamini! |
9. | Efraimu atakuwa ukiwa siku ya kukemewa; katika kabila za Israeli nimetangaza habari itakayotokea halafu bila shaka. |
10. | Wakuu wa Yuda ni kama watu waondoao alama ya mpaka; nitawamwagia ghadhabu yangu kama maji. |
11. | Efraimu ameonewa, amesetwa katika hukumu, kwa sababu alikuwa radhi kufuata ubatili. |
12. | Kwa sababu hiyo mimi nimekuwa kama nondo kwa Efraimu, nimekuwa kama ubovu kwa nyumba ya Yuda. |
13. | Efraimu alipouona ugonjwa wake, na Yuda jeraha yake, ndipo Efraimu alipokwenda kwa Ashuru, akatuma watu kwa mfalme Yarebu; lakini yeye hawezi kuwapoza, wala hatawaponya jeraha yenu. |
14. | Maana mimi nitakuwa kama simba kwa Efraimu, na kama mwana-simba kwa nyumba ya Yuda; mimi, naam, mimi nitararua, kisha nitakwenda zangu; nitachukulia mbali, wala hapatakuwa na mtu wa kupokonya. |
15. | Nitakwenda zangu niparudie mahali pangu, hata watakapoungama makosa yao na kunitafuta uso wangu; katika taabu yao watanitafuta kwa bidii. |
← Hosea (5/14) → |