← Habakkuk (3/3) |
1. | Sala ya nabii Habakuki. |
2. | Ee Bwana, nimesikia habari zako, nami naogopa; Ee Bwana, fufua kazi yako katikati ya miaka; Katikati ya miaka tangaza habari yake; Katika ghadhabu kumbuka rehema. |
3. | Mungu alikuja kutoka Temani, Yeye aliye mtakatifu kutoka mlima Parani. Utukufu wake ukazifunika mbingu, Nayo dunia ikajaa sifa yake. |
4. | Mwangaza wake ulikuwa kama nuru; Alikuwa na mishale ya nuru ubavuni pake; Ndipo ulipofichwa uweza wake. |
5. | Mbele zake ilikwenda tauni, Na makaa ya moto yakatoka miguuni pake. |
6. | Akasimama, akaitetemesha dunia; Akatazama, akawasitusha mataifa; Na milima ya zamani ikatawanyika; Vilima vya kale vikainama; Miendo yake ilikuwa kama siku za kale. |
7. | Naliziona hema za Kushani katika taabu; Mapazia ya nchi ya Midiani yakatetemeka. |
8. | Je! Bwana aliikasirikia mito? Je! Hasira yako ilikuwa juu ya mito, Au ghadhabu yako juu ya bahari, Hata ukapanda farasi zako, Katika magari yako ya wokovu? |
9. | Uta wako ukafanywa wazi kabisa; Viapo walivyopewa kabila vilikuwa neno thabiti; Ukaipasua nchi kwa mito. |
10. | Milima ilikuona, ikaogopa; Gharika ya maji ikapita; Vilindi vikatoa sauti yake, Vikainua juu mikono yake. |
11. | Jua na mwezi vikasimama makaoni mwao; Mbele ya nuru ya mishale yako ilipotapakaa, Mbele ya mwangaza wa mkuki wako umeremetao. |
12. | Ulikwenda katikati ya nchi kwa ghadhabu; Ukawapura mataifa kwa hasira. |
13. | Ukatokea kwa ajili ya wokovu wa watu wako, Kwa ajili ya wokovu wa masihi |
14. | Ukakichoma kichwa cha mashujaa wake kwa fimbo zao wenyewe; Wakaja kama kisulisuli ili kunitawanya; Kama wakifurahi kuwameza maskini kwa siri. |
15. | Ukaikanyaga bahari kwa farasi zako, Chungu ya maji yenye nguvu. |
16. | Nikasikia, na tumbo langu likatetemeka, Midomo yangu ikatikisika kwa sauti ile; Ubovu ukaingia mifupani mwangu, Nikatetemeka katika mahali pangu; Ili nipate kuingoja ile siku ya dhiki, Kundi lao washambuliao wakweapo juu ya watu. |
17. | Maana mtini hautachanua maua, Wala mizabibuni hamtakuwa na matunda; Taabu ya mzeituni itakuwa bure, Na mashamba hayatatoa chakula; Zizini hamtakuwa na kundi, Wala vibandani hamtakuwa na kundi la ng'ombe; |
18. | Walakini nitamfurahia Bwana Nitamshangilia Mungu wa wokovu wangu. |
19. | YEHOVA, aliye Bwana, ni nguvu zangu, Yeye huifanya miguu yangu kuwa kama ya kulungu, Naye ataniendesha katika mahali pangu palipoinuka. |
← Habakkuk (3/3) |