← Genesis (3/50) → |
1. | Basi nyoka alikuwa mwerevu kuliko wanyama wote wa mwitu aliowafanya Bwana Mungu. Akamwambia mwanamke, Ati! Hivi ndivyo alivyosema Mungu, Msile matunda ya miti yote ya bustani? |
2. | Mwanamke akamwambia nyoka, Matunda ya miti ya bustanini twaweza kula; |
3. | lakini matunda ya mti ulio katikati ya bustani Mungu amesema, Msiyale wala msiyaguse, msije mkafa. |
4. | Nyoka akamwambia mwanamke, Hakika hamtakufa, |
5. | kwa maana Mungu anajua ya kwamba siku mtakayokula matunda ya mti huo, mtafumbuliwa macho, nanyi mtakuwa kama Mungu, mkijua mema na mabaya. |
6. | Mwanamke alipoona ya kuwa ule mti wafaa kwa chakula, wapendeza macho, nao ni mti wa kutamanika kwa maarifa, basi alitwaa katika matunda yake akala, akampa na mumewe, naye akala. |
7. | Wakafumbuliwa macho wote wawili wakajijua kuwa wa uchi, wakashona majani ya mtini, wakajifanyia nguo. |
8. | Kisha wakasikia sauti ya Bwana Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga; Adamu na mkewe wakajificha kati ya miti ya bustani, Bwana Mungu asiwaone. |
9. | Bwana Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? |
10. | Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha. |
11. | Akasema, Ni nani aliyekuambia ya kuwa u uchi? Je! Umekula wewe matunda ya mti niliyokuagiza usiyale? |
12. | Adamu akasema, Huyo mwanamke uliyenipa awe pamoja nami ndiye aliyenipa matunda ya mti huo, nikala. |
13. | Bwana Mungu akamwambia mwanamke, Nini hili ulilolifanya? Mwanamke akasema, Nyoka alinidanganya, nikala. |
14. | Bwana Mungu akamwambia nyoka, Kwa sababu umeyafanya hayo, umelaaniwa wewe kuliko wanyama wote, na kuliko hayawani wote walioko mwituni; kwa tumbo utakwenda, na mavumbi utakula siku zote za maisha yako; |
15. | nami nitaweka uadui kati yako na huyo mwanamke, na kati ya uzao wako na uzao wake; huo utakuponda kichwa, na wewe utamponda kisigino. |
16. | Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala. |
17. | Akamwambia Adamu, Kwa kuwa umeisikiliza sauti ya mke wako, ukala matunda ya mti ambao nalikuagiza, nikisema, Usiyale; ardhi imelaaniwa kwa ajili yako; kwa uchungu utakula mazao yake siku zote za maisha yako; |
18. | michongoma na miiba itakuzalia, nawe utakula mboga za kondeni; |
19. | kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi. |
20. | Adamu akamwita mkewe jina lake Hawa; kwa kuwa yeye ndiye aliye mama yao wote walio hai. |
21. | Bwana Mungu akawafanyia Adamu na mkewe mavazi ya ngozi, akawavika. |
22. | Bwana Mungu akasema, Basi, huyu mtu amekuwa kama mmoja wetu, kwa kujua mema na mabaya; na sasa asije akanyosha mkono wake akatwaa matunda ya mti wa uzima, akala, akaishi milele; |
23. | kwa hiyo Bwana Mungu akamtoa katika bustani ya Edeni, ailime ardhi ambayo katika hiyo alitwaliwa. |
24. | Basi akamfukuza huyo mtu, akaweka Makerubi, upande wa mashariki wa bustani ya Edeni, na upanga wa moto uliogeuka huko na huko, kuilinda njia ya mti wa uzima. |
← Genesis (3/50) → |