← Galatians (5/6) → |
1. | Katika ungwana huo Kristo alituandika huru; kwa hiyo simameni, wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa. |
2. | Tazama, mimi Paulo nawaambia ninyi ya kwamba, mkitahiriwa, Kristo hatawafaidia neno. |
3. | Tena namshuhudia kila mtu atahiriwaye, kwamba ni wajibu wake kuitimiza torati yote. |
4. | Mmetengwa na Kristo, ninyi mtakao kuhesabiwa haki kwa sheria; mmeanguka na kutoka katika hali ya neema. |
5. | Maana sisi kwa Roho tunalitazamia tumaini la haki kwa njia ya imani. |
6. | Maana katika Kristo Yesu kutahiriwa hakufai neno, wala kutokutahiriwa, bali imani itendayo kazi kwa upendo. |
7. | Mlikuwa mkipiga mbio vizuri; ni nani aliyewazuia msiitii kweli? |
8. | Kushawishi huku hakukutoka kwake yeye anayewaita ninyi. |
9. | Chachu kidogo huchachua donge zima. |
10. | Nina matumaini kwenu katika Bwana, ya kwamba hamtakuwa na nia ya namna nyingine. Lakini yeye anayewafadhaisha atachukua hukumu yake, awaye yote. |
11. | Nami, ndugu zangu ikiwa ninahubiri habari ya kutahiriwa, kwa nini ningali ninaudhiwa? Hapo kwazo la msalaba limebatilika! |
12. | Laiti hao wanaowatia mashaka wangejikata nafsi zao! |
13. | Maana ninyi, ndugu, mliitwa mpate uhuru; lakini uhuru wenu usiwe sababu ya kuufuata mwili, bali tumikianeni kwa upendo. |
14. | Maana torati yote imetimilika katika neno moja, nalo ni hili, Umpende jirani yako kama nafsi yako. |
15. | Lakini mkiumana na kulana, angalieni msije mkaangamizana. |
16. | Basi nasema, Enendeni kwa Roho, wala hamtazitimiza kamwe tamaa za mwili. |
17. | Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka. |
18. | Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria. |
19. | Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi, |
20. | ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, |
21. | husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo, katika hayo nawaambia mapema, kama nilivyokwisha kuwaambia, ya kwamba watu watendao mambo ya jinsi hiyo hawataurithi ufalme wa Mungu. |
22. | Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, |
23. | upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria. |
24. | Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake. |
25. | Tukiishi kwa Roho, na tuenende kwa Roho. |
26. | Tusijisifu bure, tukichokozana na kuhusudiana. |
← Galatians (5/6) → |