← Ezra (4/10) → |
1. | Basi adui za Yuda na Benyamini, waliposikia ya kuwa wana wa uhamisho wanamjengea Bwana, Mungu wa Israeli, hekalu, |
2. | wakamkaribia Zerubabeli, na wakuu wa mbari za mababa, wakawaambia, Na tujenge sisi nasi pamoja nanyi; kwa maana tunamtafuta Mungu wenu kama ninyi, nasi twamtolea dhabihu tangu zamani za Esar-hadoni, mfalme wa Ashuru, aliyetupandisha mpaka hapa. |
3. | Lakini Zerubabeli, na Yoshua, na wakuu wengine wa mbari za mababa katika Israeli, wakawaambia, Ninyi haiwahusu kushirikiana nasi katika kumjengea Mungu wetu nyumba; bali sisi wenyewe peke yetu tutamjengea Bwana, Mungu wa Israeli, nyumba, kama mfalme Koreshi, mfalme wa Uajemi, alivyotuamuru. |
4. | Ndipo watu wa nchi wakaidhoofisha mikono ya watu wa Yuda, wakawasumbua, walipokuwa wakijenga. |
5. | Wakawaajiri washauri juu yao, ili kuwapinga kusudi lao, siku zote za Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata wakati wa kutawala kwake Dario, mfalme wa Uajemi. |
6. | Tena, wakati wa kutawala kwake Ahasuero, mwanzo wa kutawala kwake, watu wakaandika mashitaka juu ya wenyeji wa Yuda na Yerusalemu. |
7. | Na tena, katika siku za Artashasta, Mithredathi, na Tabeeli na mabaki ya wenziwe, wakimwandikia Artashasta, mfalme wa Uajemi, salamu za heri; na mwandiko wa waraka huo, ukaandikwa kwa herufi za Kiaramu, na kunenwa kwa lugha ya Kiaramu. |
8. | Nao Rehumu, Bwana shauri, na Shimshai, mwandishi, wakaandika waraka juu ya Yerusalemu kwa Artashasta, mfalme, kama hivi; |
9. | Rehumu, Bwana shauri, na Shimshai, mwandishi, na mabaki ya wenzao, makadhi wa Kiajemi na madiwani wa Kiajemi; na Waarkewi, Wababeli, Washushani, yaani, Waelami; |
10. | na mabaki ya mataifa, ambao Asur-bani-pali mkuu, mwenye heshima, aliwavusha, na kuwakalisha katika mji wa Samaria, na mahali penginepo, ng'ambo ya Mto; wakadhalika. |
11. | Hii ndiyo nakili ya waraka waliyompelekea mfalme Artashasta; |
12. | Ijulikane kwa mfalme ya kuwa Wayahudi, waliokwea kutoka kwako, wamefika kwetu Yerusalemu; nao wanaujenga ule mji mwasi, mbaya; wamemaliza kuta zake, na kuitengeneza misingi yake. |
13. | Basi, ijulikane kwa mfalme, ya kuwa mji huu ukijengwa, na kuta zake zikimalizika, hawatatoa kodi, wala ada, wala ushuru, na mwisho wake wafalme watapata hasara. |
14. | Na sisi, kwa kuwa tunakula chumvi ya nyumba ya mfalme, wala si wajibu wetu kumwona mfalme akivunjiwa heshima, basi tumetuma watu na kumwarifu mfalme. |
15. | Ili habari zitafutwe katika kitabu cha tarehe za baba zako; ndivyo utakavyopata kujua kwa kitabu cha tarehe ya kuwa mji huo ni mji mwasi, wenye kuwadhuru wafalme, na maliwali, na ya kuwa wenyeji wake wamefanya fitina katika mji huo zamani; ndiyo sababu mji huo ukaangamizwa. |
16. | Twamwarifu mfalme ya kuwa mji huo ukijengwa, na kuta zake zikimalizika, hutakuwa na sehemu ya nchi ng'ambo ya Mto. |
17. | Ndipo mfalme akapeleka majibu; |
18. | Ule waraka mlionipelekea umesomwa mbele yangu, nami nikaelewa na maana yake. |
19. | Nikatoa amri, na watu wametafuta habari; ikaonekana ya kuwa mji huu zamani umefanya fitina juu ya wafalme, na ya kuwa uasi na fitina zimefanyika ndani yake. |
20. | Tena walikuwako wafalme wakuu juu ya Yerusalemu, waliotawala nchi yote iliyo ng'ambo ya Mto; wakapewa kodi, na ada, na ushuru. |
21. | Sasa toeni amri kuwakomesha watu hawa kazi yao, mji huu usijengwe, hata mimi nitakapotoa amri. |
22. | Tena jihadharini, msilegee katika jambo hili; kwa nini madhara yazidi, na wafalme wapate hasara? |
23. | Hata nakala ya waraka huo wa mfalme Artashasta uliposomwa mbele ya Rehumu, Bwana shauri, na Shimshai, mwandishi, na wenzao, wakaenda Yerusalemu upesi, kwa Wayahudi, wakawakomesha kwa nguvu na kwa kuwashurutisha. |
24. | Hivyo kazi ya nyumba ya Mungu iliyoko Yerusalemu ikakoma; nayo ikakoma hata mwaka wa pili wa kutawala kwake Dario, mfalme wa Uajemi. |
← Ezra (4/10) → |