← Exodus (7/40) → |
1. | Bwana akamwambia Musa, Angalia, nimekufanya wewe kuwa kama Mungu kwa Farao; na huyo ndugu yako Haruni atakuwa nabii wako. |
2. | Utanena hayo yote nikuagizayo; na ndugu yako Haruni atanena na Farao, ili awape wana wa Israeli ruhusa watoke nchi yake. |
3. | Nami nitaufanya mgumu moyo wa Farao, nami nitazifanya kuwa nyingi ishara zangu na ajabu zangu katika nchi ya Misri. |
4. | Lakini Farao hatawasikiza ninyi, nami nitaweka mkono wangu juu ya Misri, na kuyatoa majeshi yangu, watu wangu, hao wana wa Israeli, watoke nchi ya Misri kwa hukumu zilizo kuu. |
5. | Na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, hapo nitakapounyosha mkono wangu juu ya Misri na kuwatoa wana wa Israeli watoke kati yao. |
6. | Musa na Haruni wakafanya vivyo; kama Bwana alivyowaambia, ndivyo walivyofanya. |
7. | Huyo Musa alikuwa ni mtu wa miaka themanini umri wake, na Haruni alikuwa ni mtu wa miaka themanini na mitatu, hapo waliponena na Farao. |
8. | Bwana akanena na Musa na Haruni, akawaambia, |
9. | Farao atakaponena nanyi, na kuwaambia, Jifanyieni miujiza; ndipo utakapomwambia Haruni, Shika fimbo yako, uibwage chini mbele ya Farao, ili iwe nyoka. |
10. | Basi Musa na Haruni wakaingia kwa Farao, wakafanya vivyo kama Bwana alivyowaambia; Haruni akaibwaga fimbo yake chini mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake, ikawa nyoka. |
11. | Ndipo Farao naye akawaita wenye akili na wachawi; na hao waganga wa Misri wakafanya vivyo kwa uganga wao. |
12. | Wakabwaga chini kila mtu fimbo yake, nazo zikawa nyoka; lakini fimbo ya Haruni ikazimeza fimbo zao. |
13. | Moyo wa Farao ukawa ni mgumu asiwasikize; kama Bwana alivyonena. |
14. | Bwana akamwambia Musa, Moyo wa Farao ni mzito, anakataa kuwapa watu ruhusa waende zao. |
15. | Mwendee Farao asubuhi; tazama, atoka kwenda majini; nawe simama karibu na ufuo wa mto ili upate kuonana naye; na ile fimbo iliyogeuzwa kuwa nyoka utaichukua mkononi mwako. |
16. | Nawe umwambie, Bwana, Mungu wa Waebrania, amenituma nije kwako, kusema, Wape watu wangu ruhusa, ili wapate kunitumikia jangwani; nawe, tazama! Hujasikia hata sasa. |
17. | Bwana asema, Katika jambo hili utanijua ya kuwa mimi ndimi Bwana; tazama, nitayapiga haya maji yaliyo mtoni kwa fimbo hii niliyo nayo mkononi mwangu, nayo yatageuzwa kuwa damu. |
18. | Na hao samaki walio mtoni watakufa, na huo mto utatoa uvundo; nao Wamisri watachukizwa kuyanywa maji ya mtoni. |
19. | Bwana akamwambia Musa, Mwambie Haruni, Shika fimbo yako, kaunyoshe mkono wako juu ya maji ya Misri, juu ya mito yao, juu ya vijito vyao, na juu ya maziwa ya maji yao, na juu ya visima vyao vyote vya maji, ili yageuke kuwa damu, nako kutakuwa na damu katika nchi yote ya Misri, katika vyombo vya mti, na katika vyombo vya jiwe. |
20. | Musa na Haruni wakafanya hivyo, kama Bwana alivyowaambia; naye akaiinua ile fimbo, na kuyapiga maji yaliyokuwa mtoni, mbele ya Farao, mbele ya watumishi wake; na hayo maji yote yaliyokuwa katika mto yakageuzwa kuwa damu. |
21. | Hao samaki waliokuwa mtoni nao wakafa; na ule mto ukatoa uvundo, Wamisri wasipate kunywa maji ya mtoni; na ile damu ilikuwa katika nchi yote na Misri. |
22. | Lakini waganga wa Misri wakafanya mfano wa hayo kwa uganga wao; na moyo wake Farao ukawa mgumu, wala hakuwasikiza, kama Bwana alivyonena. |
23. | Farao akazunguka na kuingia nyumbani mwake, wala hata hilo hakuliweka moyoni. |
24. | Wamisri wote wakachimba-chimba kando ya mto ili wapate maji ya kunywa; maana, hawakuweza kuyanywa yale maji ya mtoni. |
25. | Zikatimia siku saba, baada ya Bwana kuupiga ule mto. |
← Exodus (7/40) → |