← Exodus (6/40) → |
1. | Bwana akamwambia Musa, Sasa utaona nitakavyomtenda Farao; maana kwa mkono hodari atawapa ruhusa kwenda zao, na kwa mkono hodari atawafukuza katika nchi yake. |
2. | Kisha Mungu akasema na Musa, akamwambia, Mimi ni YEHOVA; |
3. | nami nilimtokea Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, kama Mungu Mwenyezi, bali kwa jina langu YEHOVA sikujulikana kwao. |
4. | Tena nimelithibitisha agano langu nao, la kuwapa nchi ya Kanaani; nchi ya kukaa kwao hali ya ugeni. |
5. | Na zaidi ya hayo, nimesikia kuugua kwao wana wa Israeli, ambao Wamisri wanawatumikisha, nami nimelikumbuka agano langu. |
6. | Basi waambie wana wa Israeli, Mimi ni YEHOVA, nami nitawatoa ninyi mtoke chini ya mizigo ya Wamisri, nami nitawaokoa na utumwa wao, nami nitawakomboa kwa mkono ulionyoshwa, na kwa hukumu kubwa; |
7. | nami nitawatwaeni kuwa watu wangu, nitakuwa Mungu kwenu; nanyi mtajua ya kuwa mimi ni YEHOVA, Mungu wenu, niwatoaye mtoke chini ya mizigo ya Wamisri. |
8. | Nami nitawaleta hata nchi ile ambayo naliinua mkono wangu, niwape Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo; nitawapa iwe urithi wenu; Mimi ni YEHOVA. |
9. | Musa akawaambia wana wa Israeli maneno haya; lakini hawakumsikiliza Musa kwa ajili ya uchungu wa moyo, na kwa ajili ya utumwa mgumu. |
10. | Bwana akasema na Musa, akamwambia, |
11. | Ingia ndani, ukaseme na Farao, mfalme wa Misri, ili awape ruhusa wana wa Israeli watoke nchi yake. |
12. | Musa akanena mbele ya Bwana, akasema, Tazama, hao wana wa Israeli hawakunisikiza mimi; basi huyo Farao atanisikizaje, mimi niliye na midomo isiyo tohara? |
13. | Bwana akanena na Musa na Haruni, akawaagiza wawaendee wana wa Israeli, na Farao, mfalme wa Misri, ili awatoe hao wana wa Israeli katika nchi ya Misri. |
14. | Hawa ndio vichwa vya nyumba za baba zao: wana wa Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Israeli; ni Hanoki, na Palu, na Hesroni, na Karmi; hao ni jamaa za Reubeni. |
15. | Na wana wa Simeoni; ni Yemueli, na Yamini, na Ohadi, na Yakini, na Sohari, na Shauli mwana wa mwanamke wa Kikanaani; hao ni jamaa za Simeoni. |
16. | Na haya ndiyo majina ya wana wa Lawi, sawasawa na vizazi vyao; Gershoni, na Kohathi, na Merari; na miaka ya maisha yake Lawi ilikuwa ni miaka mia na thelathini na saba. |
17. | Wana wa Gershoni; ni Libni, na Shimei, sawasawa na jamaa zao. |
18. | Na wana wa Kohathi; ni Amramu, na Ishari, na Hebroni, na Uzieli; na miaka ya maisha ya huyo Kohathi ilikuwa ni miaka mia na thelathini na mitatu. |
19. | Na wana wa Merari; ni Mali, na Mushi. Hizi ni jamaa za hao Walawi sawasawa na vizazi vyao. |
20. | Huyo Amramu akamwoa Yokebedi ndugu ya baba yake; naye akamzalia Haruni, na Musa; na miaka ya maisha yake Amramu ilikuwa ni miaka mia na thelathini na saba. |
21. | Na wana wa Ishari; ni Kora, na Nefegi, na Zikri. |
22. | Na wana wa Uzieli; ni Mishaeli, na Elisafani, na Sithri. |
23. | Haruni akamwoa Elisheba, binti ya Aminadabu, umbu lake Nashoni; naye akamzalia Nadabu, na Abihu, na Eleazari, na Ithamari. |
24. | Na wana wa Kora; ni Asiri, na Elkana, na Abiasafu; hizo ni jamaa za hao Wakora. |
25. | Na Eleazari mwana wa Haruni akamwoa mmoja miongoni mwa binti za Putieli; naye akamzalia Finehasi. Hawa ndio vichwa vya nyumba za mababa ya Walawi sawasawa na jamaa zao. |
26. | Hawa ni Haruni ye yule, na Musa ye yule, Bwana aliowaambia, akisema, Watoeni wana wa Israeli watoke nchi ya Misri sawasawa na majeshi yao. |
27. | Ni hao walionena na Farao mfalme wa Misri ili wawatoe wana wa Israeli watoke Misri; hao ni Musa ye yule, na Haruni ye yule. |
28. | Ilikuwa siku hiyo Bwana aliponena na Musa katika nchi ya Misri, |
29. | Bwana akamwambia Musa, akasema, Mimi ni Bwana; mwambie Farao mfalme wa Misri maneno yote nikuambiayo. |
30. | Musa akanena mbele ya Bwana, Mimi ni mtu mwenye midomo isiyo tohara, Farao atanisikizaje? |
← Exodus (6/40) → |