← Exodus (21/40) → |
1. | Basi hukumu utakazoziweka mbele ya watu ni hizi |
2. | Ukimnunua mtumwa wa Kiebrania, atakutumikia muda wa miaka sita; mwaka wa saba atatoka kwako huru bure. |
3. | Kwamba aliingia kwako peke yake tu, atatoka hivyo peke yake; kwamba ameoa, mkewe atatoka aende pamoja naye. |
4. | Kwamba ni bwana wake aliyempa huyo mke, naye amemzalia wana, wa kiume au wa kike; yule mke na wanawe watakuwa ni mali ya bwana wake, naye mume atatoka peke yake. |
5. | Lakini huyo mtumwa akisema waziwazi, Mimi nampenda bwana wangu, na mke wangu na watoto wangu; sitaki mimi kutoka niwe huru; |
6. | ndipo hapo huyo bwana wake atamleta mbele ya Mungu na kumleta mlangoni, au penye mwimo wa mlango; na bwana wake atalitoboa sikio lake kwa uma; ndipo atamtumikia sikuzote. |
7. | Mtu akimwuza binti yake awe kijakazi, hatatoka yeye kama watumwa wa kiume watokavyo. |
8. | Kwamba bwana wake hakupendezewa naye, akiwa amemposa, ndipo atakubali akombolewe; hana amri yeye kumwuza aende kwa watu wageni maana amemtenda kwa udanganyifu. |
9. | Kwamba amposa mwanawe, atamtendea kama desturi zipasazo binti zake. |
10. | Kwamba ajitwalia mke mwingine, chakula chake huyo, na nguo zake, na ngono yake, hatampunguzia. |
11. | Kwamba hamfanyii mambo haya matatu, ndipo atatoka aende bure, pasipo kutolewa mali. |
12. | Mtu awaye yote ampigaye mtu, hata akafa, hana budi atauawa huyo. |
13. | Lakini kama hakumvizia, ila Mungu amemtia mkononi mwake; basi nitakuonyesha mahali atakapopakimbilia. |
14. | Lakini, mtu akimwendea mwenziwe kwa kujikinai, kusudi apate kumwua kwa hila; huyo utamwondoa hata madhabahuni pangu, auawe. |
15. | Ampigaye baba yake au mama yake, sharti atauawa. |
16. | Yeye amwibaye mtu, na kumwuza, au akipatikana mkononi mwake, sharti atauawa huyo |
17. | Yeye amwapizaye baba yake au mama yake, sharti atauawa. |
18. | Watu wakigombana, na mmoja akimpiga mwenziwe kwa jiwe, au kwa konde, asife, lakini yualazwa kitandani mwake; |
19. | atakapoinuka tena na kuenenda nje kwa kutegemea fimbo, ndipo hapo yule aliyempiga ataachwa; ila atamlipa kwa ajili ya hayo majira yake yaliyompotea, naye atamwuguza hata apone kabisa. |
20. | Mtu akimpiga mtumwa wake, au kijakazi chake, kwa fimbo, naye akifa mkononi mwake, hana budi ataadhibiwa. |
21. | Lakini akipona siku moja au mbili hataadhibiwa; maana, ni mali yake. |
22. | Watu waume wakiteta pamoja, wakamwumiza mwanamke mwenye mimba hata akaharibu mimba, tena yasiwe madhara zaidi; sharti atatozwa mali kama atakavyomwandikia mumewe huyo mwanamke; atalipa kama hao waamuzi watakavyosema. |
23. | Lakini kwamba pana madhara zaidi, ndipo utatoza uhai kwa uhai, |
24. | jicho kwa jicho, jino kwa jino, mkono kwa mkono, mguu kwa mguu, |
25. | kuteketeza kwa kuteketeza, jeraha kwa jeraha, chubuko kwa ajili ya chubuko. |
26. | Mtu akimpiga mtumwa wake jicho, au jicho la kijakazi chake, na kuliharibu; atamwacha huru kwa ajili ya jicho lake. |
27. | Au akimpiga mtumwa wake jino likang'oka, au jino la kijakazi chake, atamwacha huru kwa ajili ya jino lake. |
28. | Ng'ombe akipiga pembe mtu mume au mtu mke, nao wakafa, huyo ng'ombe atauawa kwa kupigwa kwa mawe, nyama yake isiliwe; lakini mwenye huyo ng'ombe ataachiliwa. |
29. | Lakini kwamba huyo ng'ombe alizoea kupiga watu tangu hapo, naye mwenyewe ameonyeshwa jambo hilo, wala asimzuie, naye amemwua mtu mume au mwanamke; huyo ng'ombe atauawa kwa kupigwa kwa mawe, na huyo mwenyewe naye atauawa. |
30. | Lakini akiandikiwa ukombozi, ndipo atakapotoa kwa ajili ya uhai wake hicho atakachoandikiwa. |
31. | Akiwa ng'ombe amempiga pembe mtoto wa kiume na kumtumbua, au akiwa amempiga mtoto wa kike, atatendwa kama hukumu hiyo. |
32. | Ng'ombe akimtumbua mtumwa mume au kijakazi; mwenye ng'ombe atampa bwana wao shekeli thelathini za fedha, naye ng'ombe atauawa kwa kupigwa kwa mawe. |
33. | Kwamba mtu atafunua shimo, au kuchimba shimo, naye asilifunike, kisha ikawa ng'ombe au punda kutumbukia humo, |
34. | mwenye shimo atalipa; atampa huyo mwenye mnyama fedha, na mnyama aliyekufa atakuwa ni wake. |
35. | Ng'ombe wa mtu akimwumiza ng'ombe wa mtu mwingine hata akafa; ndipo watamwuza huyo ng'ombe aliye hai na kugawanya thamani yake; na ng'ombe aliyekufa pia watamgawanya. |
36. | Au kwamba ilijulikana ya kuwa ng'ombe tangu hapo amezoea kupiga kwa pembe, wala mwenyewe asimzuie; ndipo atakapolipa yeye, ng'ombe kwa ng'ombe, na huyo ng'ombe aliyekufa atakuwa ni wake. |
← Exodus (21/40) → |