← Exodus (19/40) → |
1. | Mwezi wa tatu baada ya kutoka Waisraeli katika nchi ya Misri, siku iyo hiyo wakafika jangwa la Sinai. |
2. | Nao walipokuwa wameondoka Refidimu na kufika jangwa la Sinai, wakatua katika lile jangwa; Israeli wakapiga kambi huko wakiukabili mlima. |
3. | Musa akapanda kwa Mungu, na Bwana akamwita toka mlima ule, akisema, Utawaambia nyumba ya Yakobo, na kuwaarifu wana wa Israeli, maneno haya; |
4. | Mmeona jinsi nilivyowatendea Wamisri, na jinsi nilivyowachukua ninyi juu ya mbawa za tai, nikawaleta ninyi kwangu mimi. |
5. | Sasa basi ikiwa mtaitii sauti yangu kweli kweli, na kulishika agano langu, hapo ndipo mtakapokuwa tunu kwangu kuliko makabila yote ya watu; maana dunia yote pia ni mali yangu, |
6. | nanyi mtakuwa kwangu ufalme wa makuhani, na taifa takatifu. Hayo ndiyo maneno utakayowaambia wana wa Israeli. |
7. | Musa akaenda akawaita wazee wa watu, akawafunulia maneno hayo yote, Bwana aliyokuwa amemwagiza. |
8. | Watu wote wakaitika pamoja wakisema, Hayo yote aliyoyasema Bwana tutayatenda. Naye Musa akamwambia Bwana maneno ya hao watu. |
9. | Bwana akamwambia Musa, Tazama, mimi naja kwako katika wingu zito ili watu hawa wasikie nitakaposema nawe, nao wapate kukuamini wewe nawe hata milele. Musa akamwambia Bwana hayo maneno ya watu. |
10. | Bwana akamwambia Musa, Enenda kwa watu hawa, ukawatakase leo na kesho, wakazifue nguo zao, |
11. | wawe tayari kwa siku ya tatu; maana siku ya tatu Bwana atashuka katika mlima wa Sinai machoni pa watu hawa wote. |
12. | Nawe utawawekea mipaka watu hawa pande zote, ukisema, Jihadharini, msipande mlima huu, wala msiuguse, hata mapambizo yake; kila mtu atakayeugusa mlima huu, bila shaka atauawa. |
13. | Mkono wa mtu awaye yote usimguse mtu huyo, ila hakika yake atapigwa kwa mawe, au kupigwa kwa mkuki; kwamba ni mnyama au kwamba ni mwanadamu, hataishi. Hapo panda itakapotoa sauti kwa kufuliza ndipo watakapoukaribia mlima. |
14. | Musa akatelemka mlimani akawaendea watu akawatakasa, nao wakafua nguo zao. |
15. | Akawaambia watu; Mwe tayari siku ya tatu; msimkaribie mwanamke. |
16. | Ikawa siku ya tatu, wakati wa asubuhi, palikuwa na ngurumo na umeme, na wingu zito juu ya mlima, na sauti ya baragumu iliyolia sana. Watu wote waliokuwa kituoni wakatetemeka. |
17. | Musa akawatoa hao watu katika kituo, akawaleta ili waonane na Mungu; wakasimama pande za chini za kile kilima. |
18. | Mlima wa Sinai wote pia ukatoa moshi, kwa sababu Bwana alishuka katika moto; na ule moshi wake ukapanda juu kama moshi wa tanuu, mlima wote ukatetemeka sana. |
19. | Na hapo sauti ya baragumu ilipozidi kulia sana, Musa akanena, naye Mungu akamwitikia kwa sauti. |
20. | Bwana akaushukia mlima, juu ya kilele cha mlima; Bwana akamwita Musa aende hata kilele cha mlima; Musa akapanda juu. |
21. | Ndipo Bwana akamwambia Musa, Shuka chini, uwaonye watu wasije wakapasua njia waje kwa Bwana kutazama, kisha wengi miongoni mwao wakaangamia. |
22. | Makuhani nao, wamkaribiao Bwana, na wajitakase, Bwana asije akawafurikia. |
23. | Musa akamwambia Bwana, Watu hawa hawawezi kuukaribia mlima wa Sinai; kwa kuwa wewe ulituusia, ukisema, Wekeni mipaka kando-kando ya mlima, na kuutenga. |
24. | Bwana akamwambia, Nenda, ushuke wewe; nawe utakwea, wewe, na Haruni pamoja nawe; lakini wale makuhani na watu wasipenye kumkaribia Bwana, asije yeye akawafurikia juu yao. |
25. | Basi Musa akawatelemkia hao watu na kuwaambia hayo. |
← Exodus (19/40) → |