← Ephesians (6/6) |
1. | Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki. |
2. | Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi, |
3. | Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia. |
4. | Nanyi, akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana. |
5. | Enyi watumwa, watiini wao walio bwana zenu kwa jinsi ya mwili, kwa hofu na kutetemeka, kwa unyofu wa moyo, kana kwamba ni kumtii Kristo; |
6. | wala si kwa utumwa wa macho tu kama wajipendekazao kwa wanadamu bali kama watumwa wa Kristo, mkitenda yampendezayo Mungu kwa moyo; |
7. | kwa nia njema kama kumtumikia Bwana wala si mwanadamu; |
8. | mkijua ya kuwa kila neno jema alitendalo mtu atapewa lilo hilo na Bwana kwamba ni mtumwa au kwamba ni huru. |
9. | Nanyi, akina bwana, watendeeni wao yayo hayo, mkiacha kuwaogofya, huku mkijua ya kuwa yeye aliye Bwana wao na wenu yuko mbinguni, wala kwake hakuna upendeleo. |
10. | Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. |
11. | Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani. |
12. | Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. |
13. | Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. |
14. | Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani, |
15. | na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani; |
16. | zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. |
17. | Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu; |
18. | kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote; |
19. | pia na kwa ajili yangu mimi, nipewe usemi kwa kufumbua kinywa changu, ili niihubiri kwa ujasiri ile siri ya Injili; |
20. | ambayo kwa ajili yake mimi ni mjumbe katika minyororo; hata nipate ujasiri katika huyo kunena jinsi inipasavyo kunena. |
21. | Basi ninyi nanyi mpate kuzijua habari zangu, ni hali gani, Tikiko, ndugu mpendwa, mhudumu mwaminifu katika Bwana, atawajulisheni mambo yote; |
22. | ambaye nampeleka kwenu kwa kusudi lilo hilo mpate kuzijua habari zetu, naye awafariji mioyo yenu. |
23. | Amani na iwe kwa ndugu, na pendo, pamoja na imani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Bwana Yesu Kristo. |
24. | Neema na iwe pamoja na wote wampendao Bwana wetu Yesu Kristo katika hali ya kutokuharibika. |
← Ephesians (6/6) |