← Ephesians (4/6) → |
1. | Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; |
2. | kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; |
3. | na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani. |
4. | Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. |
5. | Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. |
6. | Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote. |
7. | Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo. |
8. | Hivyo husema, Alipopaa juu aliteka mateka, Akawapa wanadamu vipawa. |
9. | Basi neno hilo, Alipaa, maana yake nini kama siyo kusema kwamba yeye naye alishuka mpaka pande zilizo chini za nchi? |
10. | Naye aliyeshuka ndiye yeye aliyepaa juu sana kupita mbingu zote, ili avijaze vitu vyote. |
11. | Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; |
12. | kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; |
13. | hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; |
14. | ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. |
15. | Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo. |
16. | Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo. |
17. | Basi nasema neno hili, tena nashuhudia katika Bwana, tangu sasa msienende kama Mataifa waenendavyo, katika ubatili wa nia zao; |
18. | ambao; akili zao zimetiwa giza, nao wamefarikishwa na uzima wa Mungu, kwa sababu ya ujinga uliomo ndani yao, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao; |
19. | ambao wakiisha kufa ganzi wanajitia katika mambo ya ufisadi wapate kufanyiza kila namna ya uchafu kwa kutamani. |
20. | Bali ninyi, sivyo mlivyojifunza Kristo; |
21. | ikiwa mlimsikia mkafundishwa katika yeye, kama kweli ilivyo katika Yesu, |
22. | mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya; |
23. | na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu; |
24. | mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli. |
25. | Basi uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake; kwa maana tu viungo, kila mmoja kiungo cha wenzake. |
26. | Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka; |
27. | wala msimpe Ibilisi nafasi. |
28. | Mwibaji asiibe tena; bali afadhali afanye juhudi, akitenda kazi iliyo nzuri kwa mikono yake mwenyewe, apate kuwa na kitu cha kumgawia mhitaji. |
29. | Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia. |
30. | Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi. |
31. | Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya; |
32. | tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi. |
← Ephesians (4/6) → |