← Deuteronomy (9/34) → |
1. | Sikiza, Ee Israeli; hivi leo unataka kuvuka Yordani uingie kwa kuwamiliki mataifa yaliyo makubwa, na yenye nguvu kukupita wewe, miji mikubwa iliyojengewa kuta hata mbinguni, |
2. | watu wakubwa, warefu, wana wa Waanaki, uwajuao, uliokuwa ukisikia wakitajwa hivi, Ni nani awezaye kusimama mbele ya wana wa Anaki? |
3. | Basi jua siku hii ya leo kuwa Bwana, Mungu wako, ndiye atanguliaye kuvuka mbele yako kama moto uteketezao; atawaangamiza, tena atawaangusha mbele yako; ndivyo utakavyowafukuza na kuwapoteza upesi, kama alivyokuambia Bwana. |
4. | Usiseme moyoni mwako, Bwana, Mungu wako, atakapokwisha kuwasukumia nje mbele yako, ukasema, Ni kwa haki yangu alivyonitia Bwana niimiliki nchi hii; kwani ni kwa ajili ya uovu wa mataifa haya Bwana awafukuza nje mbele yako. |
5. | Si kwa haki yako, wala kwa unyofu wa moyo wako, hivi uingiavyo kuimiliki nchi yao; lakini ni kwa uovu wa mataifa haya Bwana, Mungu wako, awafukuza nje mbele yako; tena apate kuliweka imara hilo neno Bwana alilowaapia baba zako Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo. |
6. | Basi jua ya kuwa Bwana, Mungu wako, hakupi nchi hii nzuri uimiliki kwa ajili ya haki yako, kwa maana u taifa lenye shingo ngumu. |
7. | Kumbuka, usisahau ulivyomtia Bwana, Mungu wako, kasirani jangwani; tangu siku uliyotoka nchi ya Misri hata mlipofika mahali hapa, mmekuwa na uasi juu ya Bwana |
8. | Tena mlimkasirisha Bwana katika Horebu, Bwana akakasirika nanyi hata akataka kuwaangamiza. |
9. | Na hapo nilipokwea mlimani kwenda kuzipokea mbao za mawe, nazo ni mbao za agano Bwana alilofanya nanyi, ndipo nikakaa mle mlimani siku arobaini usiku na mchana; sikula chakula wala kunywa maji. |
10. | Bwana akanipa zile mbao mbili za mawe zimeandikwa kwa kidole cha Mungu; na juu yake yameandikwa maneno mfano wa yote aliyosema nanyi Bwana mle mlimani toka kati ya moto siku ya mkutano. |
11. | Ikawa mwisho wa siku arobaini usiku na mchana, Bwana alinipa zile mbao mbili za mawe, nazo ni mbao za agano. |
12. | Bwana akaniambia, Ondoka huko, shuka upesi; kwa kuwa watu wako uliowatoa Misri wamejiharibu; wamekengeuka mara katika njia niliyowaamuru; wamejifanyia sanamu ya kusubu. |
13. | Tena Bwana akasema nami zaidi, akaniambia, Nimeliona taifa hili; na tazama, ni taifa lenye shingo ngumu; |
14. | niache, nipate kuwaangamiza, na kulifuta jina lao chini ya mbingu; nami nitakufanya wewe uwe taifa kubwa lenye nguvu kuwapita wao. |
15. | Basi nikageuka nikashuka mle mlimani, mlima ukawaka moto; na zile mbao mbili za agano zilikuwa katika mikono yangu miwili. |
16. | Nikaangalia, na tazama, mlikuwa mmefanya dhambi juu ya Bwana, Mungu wenu; mmefanya ndama ya ng'ombe ya kusubu; mmekengeuka upesi katika njia aliyowaamuru Bwana. |
17. | Nikazishika zile mbao mbili, nikazitupa kutoka katika mikono yangu miwili, nikazivunja mbele ya macho yenu. |
18. | Nikaanguka nchi mbele za Bwana siku arobaini usiku na mchana, kama pale kwanza; sikula chakula wala kunywa maji; kwa sababu ya makosa yenu yote mliyokosa, kwa kufanya yaliyo maovu machoni pa Bwana, kwa kumkasirisha. |
19. | Kwa kuwa niliogopa hasira na makamio aliyowakasirikia Bwana kutaka kuwaangamiza. Lakini Bwana alinisikiza wakati huo nao. |
20. | Bwana akamkasirikia sana Haruni akataka kumwangamiza; nikamwombea Haruni naye wakati huo. |
21. | Kisha nikaitwaa ile dhambi yenu, huyo ndama mliyemfanya, nikamteketeza kwa moto, nikamponda, nikamsaga tikitiki, hata akawa laini kama vumbi; nikalitupa vumbi lake katika kijito kilichoshuka kutoka mlimani. |
22. | Tena huko Tabera, na Masa, na Kibroth-hataava mlimtia Bwana hasira. |
23. | Na wakati alipowatuma Bwana kutoka Kadesh-barnea, akiwaambia, Kweeni mkaimiliki nchi niliyowapa; ndipo mkaasi juu ya maagizo ya Bwana, Mungu wenu, hamkumsadiki wala hamkusikiza sauti yake. |
24. | Mmekuwa na uasi juu ya Bwana tokea siku nilipowajua ninyi. |
25. | Ndipo nikaanguka nchi mbele za Bwana siku zile arobaini usiku na mchana nilizokuwa nimeanguka nchi; kwa kuwa Bwana alisema atawaangamiza. |
26. | Nikamwomba Bwana, nikasema, Ee Bwana Mungu, usiwaangamize watu wako, urithi wako, uliowakomboa kwa ukuu wako, uliowatoa Misri kwa mkono wa nguvu. |
27. | Wakumbuke watumwa wako, Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo; usiangalie upotofu wa watu hawa, wala uovu wao, wala dhambi yao; |
28. | isije nchi uliyotutoa ikasema, Ni kwa sababu Bwana hakuweza kuwaleta katika nchi aliyowapa ahadi, tena ni kwa kuwa aliwachukia, alivyowatoa nje ili kuwaua jangwani. |
29. | Nao ni watu wako, urithi wako, uliowatoa kwa nguvu zako kuu na mkono wako ulionyoka. |
← Deuteronomy (9/34) → |