| ← Deuteronomy (6/34) → |
| 1. | Na hii ndiyo sheria, na amri, na hukumu, alizoziamuru Bwana, Mungu wenu, mfundishwe, mpate kuzitenda katika nchi ile mnayoivukia kuimiliki; |
| 2. | upate kumcha Bwana, Mungu wako, kushika amri zake zote, na sheria zake, ninazokuamuru, wewe na mwanao, na mwana wa mwanao, siku zote za maisha yako; tena siku zako ziongezwe. |
| 3. | Sikiza basi, Ee Israeli, ukaangalie kuzitenda; upate kufanikiwa, mpate kuongezeka sana, kama Bwana, Mungu wa baba zako, alivyokuahidi, katika nchi ijaayo maziwa na asali. |
| 4. | Sikiza, Ee Israeli; Bwana, Mungu wetu, Bwana ndiye mmoja. |
| 5. | Nawe mpende Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote. |
| 6. | Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; |
| 7. | nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo. |
| 8. | Yafunge yawe dalili juu ya mkono wako, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yako. |
| 9. | Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako. |
| 10. | Tena itakuwa atakapokwisha Bwana, Mungu wako, kukuleta katika nchi aliyowaapia babu zako, Ibrahimu na Isaka na Yakobo, ya kuwa atakupa; miji mikubwa mizuri usiyoijenga wewe, |
| 11. | na nyumba zimejaa vitu vyema vyote usizojaza wewe, na visima vimefukuliwa usivyofukua wewe, mashamba ya mizabibu na mizeituni usiyoipanda wewe, nawe utakula na kushiba; |
| 12. | ndipo ujitunze, usije ukamsahau Bwana aliyekutoa nchi ya Misri, nyumba ya utumwa. |
| 13. | Mche Bwana, Mungu wako; ndiye utakayemtumikia, na kuapa kwa jina lake. |
| 14. | Msifuate miungu mingine katika miungu ya mataifa wawazungukao; |
| 15. | kwani Bwana, Mungu wako, aliye katikati yako ni Mungu mwenye wivu; isije ikawaka juu yako hasira ya Bwana, Mungu wako, akakuangamiza kutoka juu ya uso wa nchi. |
| 16. | Msimjaribu Bwana, Mungu wenu, kama mlivyomjaribu huko Masa. |
| 17. | Zishikeni kwa bidii sheria za Bwana, Mungu wenu, na mashuhudizo yake, na amri zake alizokuagiza. |
| 18. | Nawe fanya yaliyo sawa, na mema, machoni pa Bwana; ili mpate kufanikiwa, nawe upate kuingia na kuimiliki nchi nzuri Bwana aliyowaapia baba zako, |
| 19. | ya kuwa atawasukumia nje adui zako wote mbele yako, kama alivyosema Bwana. |
| 20. | Na zamani zijazo atakapokuuliza mwanao, akikuambia, N'nini mashuhudizo, na amri, na hukumu, alizowaagiza Bwana, Mungu wetu? |
| 21. | Ndipo umwambie mwanao, Tulikuwa watumwa wa Farao huko Misri; Bwana, akatutoa kutoka Misri kwa mkono wa nguvu; |
| 22. | Bwana akaonya ishara na maajabu, makubwa, mazito, juu ya Misri, na juu ya Farao, na juu ya nyumba yake yote, mbele ya macho yetu; |
| 23. | akatutoa huko ili kututia huku, apate kutupa nchi aliyowaapia baba zetu. |
| 24. | Bwana akatuamuru kuzifanya amri hizi zote, tumche Bwana, Mungu wetu, tuone mema sikuzote ili atuhifadhi hai kama hivi leo. |
| 25. | Tena itakuwa haki kwetu, tukitunza kufanya maagizo haya yote mbele ya Bwana, Mungu wetu, kama alivyotuagiza. |
| ← Deuteronomy (6/34) → |