← Deuteronomy (32/34) → |
1. | Sikilizeni, enyi mbingu, nami nitanena; Na nchi isikie maneno ya kinywa changu. |
2. | Mafundisho yangu yatadondoka kama mvua, Maneno yangu yatatona-tona kama umande; Kama manyunyu juu ya majani mabichi; Kama matone ya mvua juu ya mimea. |
3. | Maana nitalitangaza Jina la Bwana; Mpeni ukuu Mungu wetu. |
4. | Yeye Mwamba, kazi yake ni kamilifu; Maana, njia zake zote ni haki. Mungu wa uaminifu, asiye na uovu, Yeye ndiye mwenye haki na adili. |
5. | Wametenda mambo ya uharibifu, Hawawi watoto wake, hii ndiyo ila yao; Wao ni kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka. |
6. | Je! Mnamlipa Bwana hivi, Enyi watu wapumbavu na ujinga? Je! Yeye siye baba yako aliyekununua? Amekufanya, na kukuweka imara. |
7. | Kumbuka siku za kale, Tafakari miaka ya vizazi vingi; Mwulize baba yako, naye atakuonyesha; Wazee wako, nao watakuambia. |
8. | Yeye Aliye Juu alipowapa mataifa urithi wao, Alipowabagua wanadamu, Aliweka mipaka ya watu Kwa kadiri ya hesabu ya wana wa Israeli. |
9. | Maana, sehemu ya Bwana ni watu wake, Yakobo ni kura ya urithi wake. |
10. | Alimkuta katika nchi ya ukame, Na katika jangwa tupu litishalo; Alimzunguka, akamtunza; Akamhifadhi kama mboni ya jicho; |
11. | Mfano wa tai ataharikishaye kioto chake; Na kupapatika juu ya makinda yake, Alikunjua mbawa zake, akawatwaa, Akawachukua juu ya mbawa zake; |
12. | Bwana peke yake alimwongoza, Wala hapakuwa na mungu mgeni pamoja naye. |
13. | Alimpandisha mahali pa nchi palipoinuka, Naye akala mazao ya mashamba; Akamnyonyesha asali iliyotoka jabalini, Na mafuta yaliyotoka katika mwamba wa gumegume; |
14. | Siagi ya ng'ombe, na maziwa ya kondoo, Pamoja na mafuta ya wana-kondoo, Kondoo waume wa Kibashani, na mbuzi, Na unono wa ngano iliyo nzuri; Ukanywa divai, damu ya mizabibu. |
15. | Lakini Yeshuruni alinenepa, akapiga teke; Umenenepa, umekuwa mnene, umewanda; Ndipo akamwacha Mungu aliyemfanya, Akamdharau Mwamba wa wokovu wake. |
16. | Wakamtia wivu kwa miungu migeni, Wakamkasirisha kwa machukizo. |
17. | Walitoa sadaka kwa pepo, si Mungu, Kwa miungu wasiyoijua, Kwa miungu mipya iliyotokea siku zilizo karibu, Ambayo baba zenu hawakuiogopa. |
18. | Humkumbuki Mwamba aliyekuzaa, Mungu aliyekuzaa umemsahau. |
19. | Bwana akaona, akawachukia, Kwa sababu ya kukasirishwa na wanawe na binti zake. |
20. | Akasema, Nitawaficha uso wangu, Nitaona mwisho wao utakuwaje; Maana, ni kizazi cha ukaidi mwingi, Watoto wasio imani ndani yao. |
21. | Wamenitia wivu kwa kisicho Mungu; Wamenikasirisha kwa ubatili wao; Nami nitawatia wivu kwa wasio watu, Nami nitawakasirisha kwa taifa lipumbaalo. |
22. | Maana, moto umewashwa kwa hasira yangu, Unateketea hata chini ya kuzimu, Unakula dunia pamoja na mazao yake, Unaunguza misingi ya milima. |
23. | Nitaweka madhara juu yao chunguchungu; Nitawapiga kwa mishale yangu hata ikaishe; |
24. | Watakonda kwa njaa, wataliwa na makaa ya moto, Na uharibifu mkali; Nitawapelekea meno ya wanyama wakali, Pamoja na sumu ya wadudu watambaao mavumbini. |
25. | Nje upanga utawafifiliza Na ndani ya vyumba, utisho; Utaangamiza mvulana na msichana, Anyonyaye pamoja na mwenye mvi, |
26. | Nalisema, Ningewatawanyia mbali, Ningekomesha kumbukumbu lao kati ya wanadamu; |
27. | Isipokuwa naliogopa makamio ya adui, Adui zao wasije wakafikiri uongo, Wasije wakasema, Mkono wetu umetukuka, Wala Bwana hakuyafanya haya yote. |
28. | Maana hawa ni taifa wasio shauri, Wala fahamu hamna ndani yao. |
29. | Laiti wangekuwa na akili, hata wakafahamu haya, Ili watafakari mwisho wao. |
30. | Mmoja angefukuzaje watu elfu, Wawili wangekimbizaje elfu kumi, Kama Mwamba wao asingaliwauza, Kama Bwana asingaliwatoa? |
31. | Maana, Mwamba wao si kama Mwamba wetu, Hata adui zetu wenyewe ndivyo wahukumuvyo. |
32. | Maana, mzabibu wao ni mzabibu wa Sodoma, Nao ni wa mashamba ya Gomora; Zabibu zao ni zabibu za uchungu, Vichala vyao ni vichungu. |
33. | Mvinyo yao ni sumu ya majoka, Uchungu mkali wa nyoka. |
34. | Je! Haya hayakuwekwa akiba kwangu? Na kutiwa muhuri kati ya hazina yangu? |
35. | Kisasi ni changu mimi, na kulipa, Wakati itakapoteleza miguu yao; Maana siku ya msiba wao imekaribia, Na mambo yatakayowapata yatafanya haraka. |
36. | Kwa kuwa Bwana atawaamua watu wake, Atawahurumia watumwa wake, Aonapo ya kuwa nguvu zao zimeondoka, Na ya kuwa habaki mtu, aliyefungwa wala asiyefungwa, |
37. | Naye atasema, Iko wapi miungu yao, Mwamba ule walioutumaini; |
38. | Uliokula shahamu za sadaka zao, Na kunywa divai ya sadaka zao za kinywaji? Na waondoke na kuwasaidia ninyi; Na wawe hao himaya yenu. |
39. | Fahamu sasa ya kuwa Mimi, naam, Mimi ndiye, Wala hapana Mungu mwingine ila Mimi; Naua Mimi, nahuisha Mimi, Nimejeruhi, tena naponya; Wala hapana awezaye kuokoa katika mkono wangu, |
40. | Maana, nainua mkono wangu mbinguni, Na kusema, Kama Mimi niishivyo milele, |
41. | Nikiunoa upanga wangu wa umeme, Mkono wangu ukishika hukumu, Nitawatoza kisasi adui zangu, Nitawalipa wanaonichukia. |
42. | Nitailevya mishale yangu kwa damu, Na upanga wangu utakula nyama; Pamoja na damu ya waliouawa na waliotekwa nyara, Katika vichwa vya wakuu wa adui. |
43. | Furahini, enyi mataifa, pamoja na watu wake; Kwa maana atatwaa kisasi kwa damu ya watumwa wake, Atawatoza kisasi adui zake, Tena atafanya kafara kwa nchi yake, na watu wake. |
44. | Musa akaja akasema maneno haya yote ya wimbo huu masikioni mwa watu, yeye na Yoshua, mwana wa Nuni. |
45. | Musa akamaliza kuwaambia Israeli wote maneno haya yote; |
46. | akawaambia, Yawekeni mioyoni mwenu maneno yote ambayo nashuhudia kwenu hivi leo; nayo waamuruni watoto wenu, wayatunze na kuyafanya maneno yote ya torati hii. |
47. | Kwa maana si jambo lisilofaa kwenu; maana, ni maisha yenu, na kwa jambo hili mtazifanya siku zenu kuwa nyingi juu ya nchi mwivukiayo Yordani kuimiliki. |
48. | Bwana akasema na Musa siku iyo hiyo, akamwambia, |
49. | Kwea katika mlima huu wa Abarimu, mpaka kilima cha Nebo, kilicho katika nchi ya Moabu, kuelekea Yeriko; ukaangalie nchi ya Kanaani niwapayo wana wa Israeli kuimiliki; |
50. | ukafe katika kilima, huko ukweako, ukusanywe uwe pamoja na jamaa zako; kama alivyokufa nduguyo Haruni katika mlima wa Hori, akakusanywa awe pamoja na watu wake; |
51. | kwa sababu mlinikosa ninyi juu yangu katikati ya wana wa Israeli katika maji ya Meriba huko Kadeshi, katika bara ya Sini; kwa kuwa hamkunitakasa katikati ya wana wa Israeli. |
52. | Kwani utaiona hiyo nchi mbele yako, lakini hutakwenda huko kuingia hiyo nchi niwapayo wana wa Israeli. |
← Deuteronomy (32/34) → |