← Deuteronomy (27/34) → |
1. | Musa na wazee wa Israeli wakawaagiza wale watu wakawaambia, Shikeni maagizo yote niwaagizayo leo. |
2. | Na iwe, siku mtakayovuka Yordani kwenda nchi akupayo Bwana, Mungu wako, ujisimamishie mawe makubwa, ukayatalize matalizo, |
3. | uyaandike maneno yote ya torati hii juu yake, utakapokwisha kuvuka; ili upate kuingia nchi akupayo Bwana, Mungu wako, nchi imiminikayo maziwa na asali, kama alivyokuahidi Bwana, Mungu wa baba zako. |
4. | Na iwe, mtakapokwisha vuka Yordani myasimamishe mawe haya, niwaagizayo hivi leo, katika mlima Ebali, nawe yatalize matalizo. |
5. | Na huko umjengee madhabahu Bwana, Mungu wako, madhabahu ya mawe, usitumie chombo cha chuma juu yake. |
6. | Jenga hiyo madhabahu ya Bwana, Mungu wako, kwa mawe yasiyochongwa; ukamtolee Bwana, Mungu wako, sadaka za kuteketezwa juu yake; |
7. | ufanye na sadaka za amani, ukale huko; nawe furahi mbele za Bwana, Mungu wako. |
8. | Kisha, andika juu ya mawe hayo maneno ya torati hii yote, waziwazi sana. |
9. | Musa na makuhani Walawi wakawaambia Israeli wote wakasema, Nyamaza, usikize, Ee Israeli; leo umekuwa watu wa Bwana, Mungu wako. |
10. | Basi isikize sauti ya Bwana, Mungu wako, ufanye maagizo yake na amri zake nikuagizavyo leo. |
11. | Musa akawaagiza wale watu siku iyo hiyo, akasema, |
12. | Hawa na wasimame juu ya mlima wa Gerizimu kwa kuwabarikia watu, mkiisha vuka Yordani; Simeoni, na Lawi, na Yuda, na Isakari, na Yusufu, na Benyamini; |
13. | na hawa na wasimame juu ya mlima wa Ebali kwa laana; Reubeni, na Gadi, na Asheri, na Zabuloni, na Dani, na Naftali. |
14. | Kisha Walawi na wajibu, wawaambie watu wote wa Israeli kwa sauti kuu, |
15. | Na alaaniwe mtu afanyaye sanamu ya kuchonga, au ya kusubu, machukizo kwa Bwana, kazi ya mikono ya fundi, akaisimamisha kwa siri. Na watu wote wajibu, waseme, Amina. |
16. | Na alaaniwe amdharauye baba yake au mama yake. Na watu wote waseme, Amina. |
17. | Na alaaniwe aondoaye mpaka wa jirani yake. Na watu wote waseme, Amina. |
18. | Na alaaniwe ampotezaye kipofu akakosa njia. Na watu wote waseme, Amina. |
19. | Na alaaniwe apotoaye hukumu ya mgeni, na yatima, na mjane aliyefiliwa na mumewe. Na watu wote waseme, Amina. |
20. | Na alaaniwe alalaye na mke wa baba yake, kwa kuwa amefunua mavazi ya babaye. Na watu wote waseme, Amina. |
21. | Na alaaniwe alalaye na mnyama wa aina yo yote. Na watu wote waseme, Amina. |
22. | Na alaaniwe alalaye na umbu lake, binti ya babaye, au binti ya mamaye. Na watu wote waseme, Amina. |
23. | Na alaaniwe alalaye na mkwewe, mamaye mkewe. Na watu wote waseme, Amina. |
24. | Na alaaniwe ampigaye mwenzake kwa siri. Na watu wote waseme Amina. |
25. | Na alaaniwe atwaaye ujira wa kumwua asiye makosa. Na watu wote waseme, Amina. |
26. | Na alaaniwe asiyeyaweka imara maneno ya torati hii kwa kuyafanya. Na watu wote waseme, Amina. |
← Deuteronomy (27/34) → |