← Daniel (10/12) → |
1. | Katika mwaka wa tatu wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, Danieli, ambaye jina lake aliitwa Belteshaza, alifunuliwa neno; na neno lile lilikuwa kweli; maana ni vita vikubwa; naye akalifahamu neno lile, akaelewa na maono hayo. |
2. | Katika siku zile mimi, Danieli, nalikuwa nikiomboleza muda wa majuma matatu kamili. |
3. | Sikula chakula kitamu, wala nyama wala divai haikuingia kinywani mwangu, wala sikujipaka mafuta kabisa, hata majuma matatu kamili yalipotimia. |
4. | Na siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kwanza, nilipokuwa kando ya ule mto mkubwa, Hidekeli; |
5. | naliinua macho yangu, nikatazama, na kumbe, mtu aliyevikwa nguo za kitani, viuno vyake vimefungwa dhahabu safi ya Ufazi; |
6. | mwili wake pia ulikuwa kama zabarajadi safi, na uso wake mfano wa umeme, na macho yake kama taa za moto, na mikono yake na miguu yake rangi yake kama shaba iliyosuguliwa sana, na sauti ya maneno yake kama sauti ya umati wa watu. |
7. | Nami, Danieli, nikaona maono haya peke yangu; maana wale watu waliokuwa pamoja nami hawakuyaona maono haya; lakini tetemeko kuu liliwashika, hata wakakimbia ili kujificha. |
8. | Basi nikaachwa peke yangu, nikaona maono haya makubwa, wala hazikubaki nguvu ndani yangu; maana uzuri wangu uligeuzwa ndani yangu kuwa uharibifu, wala sikusaziwa nguvu. |
9. | Walakini naliisikia sauti ya maneno yake; nami niliposikia sauti ya maneno yake, ndipo nikashikwa na usingizi mzito, na uso wangu umeielekea nchi. |
10. | Na tazama, mkono ukanigusa, ukaniweka juu ya magoti yangu, na vitanga vya mikono yangu. |
11. | Akaniambia, Ee Danieli, mtu upendwaye sana, yafahamu maneno nikuambiayo, ukasimame kiwima-wima; maana kwako nimetumwa sasa. Na aliponiambia neno hili, nalisimama nikitetemeka. |
12. | Ndipo akaniambia, Usiogope, Danieli; kwa maana tangu siku ile ya kwanza ulipotia moyo wako ufahamu, na kujinyenyekeza mbele za Mungu wako, maneno yako yalisikiwa; nami nimekuja kwa ajili ya maneno yako. |
13. | Lakini mkuu wa ufalme wa Uajemi alinipinga siku ishirini na moja; bali, tazama, huyo Mikaeli, mmoja wa hao wakuu wa mbele, akaja kunisaidia; nami nikamwacha huko pamoja na wafalme wa Uajemi. |
14. | Sasa nimekuja kukufahamisha mambo yatakayowapata watu wako katika siku za mwisho; maana maono hayo ni ya siku nyingi bado. |
15. | Na alipokwisha kusema nami maneno hayo, nikauelekeza uso wangu chini, nikawa bubu. |
16. | Na kumbe, mmoja mfano wa wanadamu akanigusa midomo yangu; ndipo nikafumbua kinywa changu, nikanena, nikamwambia yeye aliyesimama karibu nami, Ee Bwana wangu, kwa sababu ya maono haya huzuni zangu zimenipata tena; hata sikusaziwa nguvu. |
17. | Maana, mtumishi wa Bwana wangu huyu atawezaje kusema na Bwana wangu huyu? Kwa maana kwangu mimi, mara hazikusalia nguvu ndani yangu, wala pumzi haikusalia ndani yangu. |
18. | Kisha mmoja mfano wa mwanadamu akanigusa tena, akanitia nguvu. |
19. | Akasema, Ee mtu upendwaye sana, usiogope; amani na iwe kwako, uwe na nguvu, naam, uwe na nguvu. Aliposema nami nikapata nguvu, nikasema, Ee Bwana wangu, na aseme Bwana wangu; kwa maana umenitia nguvu. |
20. | Ndipo akasema, Je! Unajua sababu hata nikakujia? Na sasa nitarudi ili nipigane na mkuu wa Uajemi; nami nitakapotoka huku, tazama, mkuu wa Uyunani atakuja. |
21. | Lakini nitakuambia yaliyoandikwa katika maandiko ya kweli; wala hapana anisaidiaye juu ya hao ila huyo Mikaeli, mkuu wenu. |
← Daniel (10/12) → |