← 2Samuel (8/24) → |
1. | Ikawa baadaye, Daudi akawapiga Wafilisti, akawashinda; Daudi akautwaa Gathi na vijiji vyake mikononi mwa hao Wafilisti. |
2. | Akapiga Moabu, akawapima kwa kamba hali wamelazwa chini; akapima kamba mbili za kuuawa, na kamba moja nzima ya kuhifadhi hai. Wamoabi wakawa watumwa wa Daudi, wakaleta zawadi. |
3. | Tena Daudi akampiga Hadadezeri mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba, alipokwenda kujipatia tena mamlaka yake huko Mtoni. |
4. | Daudi akampokonya wapanda farasi elfu na mia saba na askari waliokwenda kwa miguu ishirini elfu; Daudi akawakata mshipa farasi wote wa magari, ila farasi wa magari mia akawasaza. |
5. | Na Washami wa Dameski walipokuja kumsaidia Hadadezeri, mfalme wa Soba, Daudi akawapiga wa Washami watu ishirini na mbili elfu. |
6. | Daudi akaweka ngome katika Shamu ya Dameski, na hao Washami wakawa watumwa wa Daudi, wakaleta zawadi. Naye Bwana akampa Daudi kushinda kila alikokwenda. |
7. | Tena Daudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizovaliwa na watumwa wa Hadadezeri, akazileta Yerusalemu. |
8. | Tena toka Tebhathi na toka Berothai, miji ya Hadadezeri, Daudi akatwaa shaba nyingi mno. |
9. | Na Tou, mfalme wa Hamathi, aliposikia ya kwamba Daudi amewapiga jeshi lote la Hadadezeri, |
10. | Tou akamtuma kwa Daudi Hadoramu mwanawe kusalimia, na kumbarikia, kwa sababu amepigana na Hadadezeri, na kumpiga; kwa maana Hadadezeri alikuwa amepigana vita juu ya Tou. Na mkononi mwake akaleta vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na vyombo vya shaba; |
11. | hivi pia mfalme Daudi akavifanya wakfu kwa Bwana, pamoja na hiyo fedha, na dhahabu alizofanya wakfu za mataifa yote aliowashinda; |
12. | za Edomu, na za Moabu, na za wana wa Amoni, na za Wafilisti, na za Amaleki, na za nyara za Hadadezeri, mwana wa Rehobu, mfalme wa Soba. |
13. | Basi Daudi akajipatia jina, aliporudi kutoka kuwapiga Waedomi katika Bonde la Chumvi, watu kumi na nane elfu. |
14. | Akaweka askari wenye kulinda ngome katika Edomu; katikati ya Edomu yote akaweka ngome, na Waedomi wote wakawa watumwa wa Daudi. Naye Bwana akampa Daudi kushinda kila alikokwenda. |
15. | Daudi akatawala juu ya Israeli wote; naye Daudi akawafanyia hukumu na haki watu wake wote. |
16. | Huyo Yoabu, mwana wa Seruya alikuwa juu ya jeshi; na Yehoshafati, mwana wa Ahiludi, mwenye kuandika tarehe; |
17. | na Sadoki, mwana wa Ahitubu, na Ahimeleki, mwana wa Abiathari walikuwa makuhani; na Shausha mwandishi; |
18. | na Benaya, mwana wa Yehoyada, alikuwa juu ya Wakerethi na Wapelethi; nao wana wa Daudi wakawa makuhani. |
← 2Samuel (8/24) → |