← 2Samuel (5/24) → |
1. | Ndipo kabila zote za Israeli wakamwendea Daudi huko Hebroni, wakasema naye, wakinena, Tazama, sisi tu mfupa wako na nyama yako. |
2. | Zamani za kale, hapo Sauli alipokuwa mfalme juu yetu, wewe ndiwe uliyewaongoza Israeli watoke nje, na kuingia ndani. Naye Bwana akakuambia, Wewe utawalisha watu wangu Israeli, nawe utakuwa mkuu juu ya Israeli. |
3. | Basi wazee wote wa Israeli wakamwendea mfalme huko Hebroni, naye mfalme Daudi akapatana nao huko Hebroni mbele za Bwana; wakamtia Daudi mafuta awe mfalme juu ya Israeli. |
4. | Daudi alikuwa amepata miaka thelathini alipoanza kutawala, akatawala miaka arobaini. |
5. | Huko Hebroni alitawala miaka saba na miezi sita; na katika Yerusalemu alitawala miaka thelathini na tatu juu ya Israeli wote na Yuda. |
6. | Kisha mfalme na watu wake wakaenda Yerusalemu ili kupigana na Wayebusi, wenyeji wa nchi ile; hao ndio waliomwambia Daudi, wakisema, Usipowaondoa vipofu, na viwete, hutaingia humu kamwe; huku wakidhania ya kuwa Daudi hawezi kuingia humo. |
7. | Lakini Daudi aliipiga ngome ya Sayuni; huu ndio mji wa Daudi. |
8. | Naye Daudi alisema siku hiyo, Yeye atakayewapiga Wayebusi, na apande kwenye mfereji wa maji, na kuwapiga viwete, na hao vipofu, ambao roho yake Daudi inawachukia. Kwa sababu hii watu husema, Wako vipofu na viwete hawawezi kuingia nyumbani. |
9. | Basi Daudi akakaa ndani ya ngome hiyo, akaiita mji wa Daudi. Kisha Daudi akajenga toka Milo na pande za ndani. |
10. | Naye Daudi akazidi kuwa mkuu; kwa maana Bwana, Mungu wa majeshi, alikuwa pamoja naye. |
11. | Kisha Hiramu, mfalme wa Tiro, akatuma wajumbe kwa Daudi, akampelekea na mierezi, na maseremala, na waashi; nao wakamjengea Daudi nyumba. |
12. | Akajua Daudi ya kwamba Bwana amemweka imara awe mfalme juu ya Israeli, na ufalme wake ameutukuza kwa ajili ya watu wake, Israeli. |
13. | Naye Daudi akazidi kujitwalia masuria na wake huko Yerusalemu baada ya kutoka Hebroni; wakazaliwa zaidi kwa Daudi wana na binti. |
14. | Na haya ndiyo majina ya hao waliozaliwa kwake huko Yerusalemu; Shamua, na Shobabu, na Nathani, na Sulemani, |
15. | na Ibhari, na Elishua; na Nefegi, na Yafia; |
16. | na Elishama, na Eliada, na Elifeleti. |
17. | Na hao Wafilisti waliposikia kwamba wamemtia Daudi mafuta ili awe mfalme juu ya Israeli, Wafilisti wote wakapanda kumtafuta Daudi; naye Daudi akapata habari, akashuka akaenda ngomeni. |
18. | Basi Wafilisti walikuwa wamekuja na kujitawanya bondeni mwa Warefai. |
19. | Basi Daudi akauliza kwa Bwana, akisema, Je! Nipande juu ya Wafilisti? Utawatia mkononi mwangu? Naye Bwana akamwambia Daudi, Panda; kwa kuwa hakika nitawatia Wafilisti mikononi mwako. |
20. | Basi Daudi akaja Baal-perasimu, naye Daudi akawapiga huko; akasema, Bwana amewafurikia adui zangu mbele yangu, kama mafuriko ya maji. Basi akapaita mahali pale Baal-perasimu. |
21. | Nao wakaziacha sanamu zao huko, na Daudi na watu wake wakaziondolea mbali. |
22. | Lakini wakapanda hao Wafilisti tena mara ya pili, wakajitawanya bondeni mwa Warefai. |
23. | Naye Daudi alipouliza kwa Bwana, alisema, Usipande; zunguka nyuma yao, ukawajie huko mbele ya miforsadi. |
24. | Kisha itakuwa, hapo utakapoisikia sauti ya kwenda katika vilele vya miforsadi, ndipo nawe ujitahidi; kwa maana ndipo Bwana ametoka mbele yako awapige jeshi la Wafilisti. |
25. | Ndivyo alivyotenda Daudi, vile vile kama Bwana alivyomwagiza; naye akawapiga Wafilisti toka Geba hata ujapo Gezeri. |
← 2Samuel (5/24) → |