← 2Samuel (21/24) → |
1. | Kulikuwa na njaa siku za Daudi muda wa miaka mitatu, mwaka kwa mwaka; naye Daudi akautafuta uso wa Bwana. Bwana akasema, Ni kwa ajili ya Sauli, na kwa nyumba yake yenye damu, kwa kuwa aliwaua hao Wagibeoni. |
2. | Ndipo mfalme akawaita Wagibeoni akawaambia; (basi Wagibeoni si wa wana wa Israeli, ila ni wa masalio ya Waamori; na wana wa Israeli walikuwa wamewaapia; lakini Sauli akatafuta kuwaua katika juhudi yake kwa ajili ya wana wa Israeli na Yuda;) |
3. | basi Daudi akawaambia hao Wagibeoni, Niwatendee nini? Na kwa tendo gani nifanye upatanisho, mpate kuubariki urithi wa Bwana? |
4. | Na hao Wagibeoni wakamwambia, Si jambo la fedha wala dhahabu lililo kati ya sisi na Sauli, au nyumba yake; wala si juu yetu kumwua mtu ye yote katika Israeli. Akasema Mtakayoyanena, ndiyo nitakayowatendea ninyi. |
5. | Wakamwambia mfalme, Yule mtu aliyetupoteza, na kutufanyia shauri la kutuharibu, tusikae katika mipaka yo yote ya Israeli, |
6. | basi, na tutolewe watu saba katika wanawe, nasi tutawatundika mbele za Bwana katika Gibeoni, katika mlima wa Bwana. Mfalme akasema, Nitawatoa. |
7. | Lakini mfalme akamwachilia Mefiboshethi, mwana wa Yonathani, mwana wa Sauli, kwa ajili ya kiapo cha Bwana kilichokuwa kati yao, yaani, kati ya Daudi na Yonathani, mwana wa Sauli. |
8. | Ila mfalme akawatwaa hao wana wawili wa Rispa, binti Aya, aliomzalia Sauli, Armoni na Mefiboshethi; na wana watano wa Merabu binti Sauli, aliomzalia Adrieli, mwana wa Barzilai, Mmeholathi; |
9. | akawatia mikononi mwa Wagibeoni, nao wakawatundika mlimani mbele za Bwana, nao wakaangamia wote saba pamoja; wakauawa siku za mavuno, za kwanza, mwanzo wa mavuno ya shayiri. |
10. | Naye Rispa, binti Aya, akatwaa nguo ya magunia akajitandikia mwambani, tangu mwanzo wa mavuno hata waliponyeshewa mvua toka mbinguni; wala hakuacha ndege wa angani kukaa juu yao mchana, wala wanyama wa mwitu usiku. |
11. | Kisha akaambiwa Daudi hayo aliyoyafanya huyo Rispa binti Aya, suria wa Sauli. |
12. | Akaenda Daudi, akaitwaa mifupa ya Sauli na mifupa ya Yonathani mwanawe mikononi mwa watu wa Yabesh-gileadi; waliyoiiba katika njia ya Bethshani, hapo Wafilisti walipowatungika, katika siku hiyo waliyomwua Sauli huko Gilboa; |
13. | naye akaileta toka huko hiyo mifupa ya Sauli, na mifupa ya Yonathani mwanawe; nao wakaizoa mifupa yao waliotundikwa. |
14. | Kisha wakaizika mifupa ya Sauli na ya Yonathani mwanawe katika nchi ya Benyamini, huko Zela, kaburini mwa Kishi babaye; wakafanya yote aliyoyaamuru mfalme. Na baadaye Mungu aliiridhia hiyo nchi. |
15. | Basi kulikuwa na vita tena kati ya Wafilisti na Israeli; Daudi akashuka mpaka Gobu, na watumishi wake pamoja naye, akapigana na Wafilisti; naye Daudi akaishiwa na nguvu. |
16. | Naye Ishi-benobu, aliyekuwa mmojawapo wa Warefai, |
17. | Lakini Abishai, mwana wa Seruya, akamsaidia, akampiga Mfilisti, akamwua. Ndipo watu wa Daudi wakamwapia, wakasema, Wewe hutatoka tena pamoja nasi kwenda vitani, usije ukaizima taa ya Israeli. |
18. | Ikawa baada ya hayo, kulikuwa na vita tena na Wafilisti huko Gobu; ndipo Sibekai, Mhushathi, alipomwua Safu, aliyekuwa mmojawapo wa Warefai. |
19. | Kulikuwa na vita tena na Wafilisti huko Gobu; na Elhanani, mwana wa Yairi, Mbethlehemi, alimwua Goliathi, Mgiti, ambaye mti wa mkuki wake ulikuwa kama mti wa mfumaji. |
20. | Kulikuwa na vita tena huko Gathi; ambako kulikuwa na mtu mrefu sana, mwenye vidole sita katika kila mkono, na vidole sita katika kila mguu, jumla yake ishirini na vinne; yeye naye alizaliwa kwa Mrefai. |
21. | Naye huyo alipowatukana Israeli, ndipo Yonathani, mwana wa Shama, nduguye Daudi, akamwua. |
22. | Hao wanne walizaliwa kwake huyo Mrefai wa Gathi; wakaanguka kwa mkono wa Daudi, na kwa mikono ya watumishi wake. |
← 2Samuel (21/24) → |