← 2Peter (3/3) |
1. | Wapenzi, waraka huu ndio wa pili niwaandikiao ninyi; katika zote mbili naziamsha nia zenu safi kwa kuwakumbusha, |
2. | mpate kuyakumbuka yale maneno yaliyonenwa zamani na manabii watakatifu, na ile amri ya Bwana na Mwokozi iliyoletwa na mitume wenu. |
3. | Mkijua kwanza neno hili ya kwamba katika siku za mwisho watakuja na dhihaka zao watu wenye kudhihaki, wafuatao tamaa zao wenyewe, |
4. | na kusema, Iko wapi ahadi ile ya kuja kwake? Kwa maana, tangu hapo babu zetu walipolala, vitu vyote vinakaa hali iyo hiyo, tangu mwanzo wa kuumbwa. |
5. | Maana hufumba macho yao wasione neno hili ya kuwa zilikuwako mbingu tangu zamani, na nchi pia, imefanyizwa kutoka katika maji, na ndani ya maji, kwa neno la Mungu; |
6. | kwa hayo dunia ile ya wakati ule iligharikishwa na maji, ikaangamia. |
7. | Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu. |
8. | Lakini, wapenzi, msilisahau neno hili, kwamba kwa Bwana siku moja ni kama miaka elfu, na miaka elfu ni kama siku moja. |
9. | Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba. |
10. | Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea. |
11. | Basi, kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa, |
12. | mkitazamia hata ije siku ile ya Mungu, na kuihimiza; ambayo katika hiyo mbingu zitafumuliwa zikiungua, na viumbe vya asili vitateketea na kuyeyuka? |
13. | Lakini, kama ilivyo ahadi yake, mnatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake. |
14. | Kwa hiyo, wapenzi, kwa kuwa mnatazamia mambo hayo, fanyeni bidii ili mwonekane katika amani kuwa hamna mawaa wala aibu mbele yake. |
15. | Nanyi uhesabuni uvumilivu wa Bwana wetu kuwa ni wokovu, kama vile na ndugu yetu mpenzi Paulo alivyowaandikia kwa hekima aliyopewa; |
16. | vile vile kama katika nyaraka zake zote pia, akitoa humo habari za mambo hayo; katika nyaraka hizo yamo mambo ambayo ni vigumu kuelewa nayo; na mambo hayo watu wasio na elimu, wasio imara, huyapotoa, kama vile wayapotoavyo na maandiko mengine, kwa uvunjifu wao wenyewe. |
17. | Basi, wapenzi mkitangulia kujua hayo, jilindeni nafsi zenu, msije mkachukuliwa na kosa la hao wahalifu mkaanguka na kuuacha uthibitifu wenu. |
18. | Lakini, kueni katika neema, na katika kumjua Bwana wetu na Mwokozi Yesu Kristo. Utukufu una yeye sasa na hata milele. |
← 2Peter (3/3) |