← 2Kings (10/25) → |
1. | Basi Ahabu alikuwa na wana sabini katika Samaria. Yehu akaandika barua, akazipeleka Samaria kwa wakuu wa Yezreeli, yaani, wazee na hao walezi wa wana wa Ahabu, kusema, |
2. | Barua hii mara ikiwawasilia, kwa kuwa mna wana wa bwana wenu pamoja nanyi, tena kwenu kuna magari na farasi, na mji wenye boma, na silaha; |
3. | basi mtazameni yeye aliye mwema na hodari miongoni mwa wana wa bwana wenu, mkamweke kitini mwa babaye, mkaipiganie nyumba ya bwana wenu. |
4. | Lakini wao wakaogopa mno, wakasema, Tazama, wafalme wawili hawakusimama mbele yake; tupateje sisi kusimama? |
5. | Kisha yeye aliyekuwa juu ya nyumba, na yeye aliyekuwa juu ya mji, na wazee, na walezi, wakatuma ujumbe kwa Yehu, wakisema, Sisi tu watumwa wako, kila neno utakalotuambia, tutalifanya; hatutamfanya mtu awaye yote kuwa mfalme; ufanye yaliyo mema machoni pako. |
6. | Ndipo akawaandikia barua ya pili, kusema, Mkiwa upande wangu, na sauti yangu mkiisikia, vitwaeni vichwa vyao hao watu, wana wa bwana wenu, mkanijie kama wakati huu kesho hapa Yezreeli. Na hao wana wa mfalme, watu sabini, walikuwako kwa wakuu wa mji waliowalea. |
7. | Ikawa, barua ilipowawasilia, waliwatwaa hao wana wa mfalme, wakawaua, watu sabini, wakatia vichwa vyao katika makapu, wakampelekea huko Yezreeli. |
8. | Akaja mjumbe, akamwambia, akasema, Wamevileta vile vichwa vya wana wa mfalme. Akasema, Viwekeni chungu mbili penye maingilio ya lango hata asubuhi. |
9. | Ikawa asubuhi, akatoka, akasimama, akawaambia watu wote, Ninyi ni wenye haki; tazameni, mimi nalifanya fitina juu ya bwana wangu, nikamwua; ila ni nani aliyewapiga hawa wote? |
10. | Jueni basi ya kwamba halianguki chini lo lote la neno la Bwana, alilolinena Bwana juu ya nyumba ya Ahabu; kwa maana Bwana ameyafanya hayo aliyoyanena kwa kinywa cha mtumishi wake Eliya. |
11. | Hivyo Yehu akawapiga wote waliosalia wa nyumba ya Ahabu katika Yezreeli, na hao wakuu wake wote, na rafiki zake, na makuhani wake, hata hakumwachia aliyesalia hata mmoja. |
12. | Akaondoka, akashika njia akaenda Samaria. Hata njiani karibu na nyumba ya kukatia manyoya kondoo, ya wachungaji. |
13. | Yehu akakutana na ndugu za Ahazia mfalme wa Yuda, akawauliza, Ni nani ninyi? Wakamjibu, Sisi tu ndugu zake Ahazia; tunashuka kuwasalimu wana wa mfalme na wana wa malkia. |
14. | Akasema, Wakamateni wa hai. Wakawakamata wa hai, wakawaua penye birika ya nyumba ya kukatia manyoya kondoo, watu arobaini na wawili; wala hakumsaza mtu wao awaye yote. |
15. | Alipotoka huko akamkuta Yehonadabu mwana wa Rekabu akija kumlaki; akamsalimu akamwambia, Je! Moyo wako umenyoka, kama moyo wangu ulivyo pamoja na moyo wako? Akajibu Yehonadabu, Ndio. Yehu akamwambia, Kama ndio, nipe mkono wako. Akampa mkono, akamkalisha pamoja naye garini. |
16. | Akasema, Fuatana nami, ukaone wivu wangu kwa Bwana. Wakampandisha garini mwake. |
17. | Naye alipofika Samaria, aliwapiga wote waliomsalia Ahabu katika Samaria, hata akamwangamiza, sawasawa na neno la Bwana alilomwambia Eliya. |
18. | Yehu akawakusanya watu wote, akawaambia, Ahabu alimtumikia Baali kidogo; bali Yehu atamtumikia sana. |
19. | Basi niitieni manabii wote wa Baali, wote wamwabuduo, na makuhani wake wote; mtu asikose kuwapo hata mmoja. Maana ninayo dhabihu kubwa ya kumtolea Baali; ye yote atakayekosa kuwapo hataishi. Lakini Yehu alifanya hayo kwa hila, ili awaharibu waliomwabudu Baali. |
20. | Yehu akasema, Takaseni kusanyiko la dini kwa Baali. Wakalitangaza. |
21. | Yehu akatuma wajumbe katika Israeli yote, nao wote waliomwabudu Baali wakaja, wala hakusalia mtu ye yote asiyekuja. Wakaingia nyumbani mwa Baali; ikajaa nyumba ya Baali tangu mlango hata mlango. |
22. | Akamwambia yule aliyekuwa juu ya hazina ya mavazi, Uwatolee mavazi wote wanaomwabudu Baali. Akawatolea mavazi. |
23. | Akaingia Yehu na Yehonadabu mwana wa Rekabu nyumbani mwa Baali, akawaambia waliomwabudu Baali, Tafuteni mkaangalie, asiwepo hapa pamoja nanyi mtu amtumikiaye Bwana, ila wamwabuduo Baali peke yao. |
24. | Wakaingia ili watoe dhabihu na sadaka za kuteketezwa. Basi Yehu alikuwa amejiwekea nje watu themanini, akasema, Mtu mmoja akiokoka wa watu niliowatia mikononi mwenu, amwachaye huyo, roho yake itakuwa badala ya roho yake. |
25. | Ikawa mara alipokwisha kutoa sadaka ya kuteketezwa, Yehu akawaambia walinzi na maakida, Ingieni mwapige; mtu awaye yote asitoke. Basi wakawapiga kwa makali ya upanga; walinzi na maakida wakawatupa nje, wakaenda mpaka mji wa nyumba ya Baali. |
26. | Wakazitoa nguzo zilizokuwamo nyumbani mwa Baali, wakaziteketeza. |
27. | Wakaibomoa nguzo ya Baali, na kuiangusha nyumba ya Baali, wakaifanya choo hata leo. |
28. | Ndivyo Yehu alivyomharibu Baali katika Israeli. |
29. | Walakini katika makosa yake Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli, Yehu hakutoka katika kuyafuata, yaani, ndama za dhahabu zilizokuwako katika Betheli na Dani. |
30. | Bwana akamwambia Yehu, Kwa kuwa umetenda vema kwa kufanya vilivyo haki machoni pangu, kuitendea nyumba ya Ahabu sawasawa na yote yaliyomo moyoni mwangu, wana wako wa kizazi cha nne watakaa kitini mwa Israeli. |
31. | Lakini Yehu hakuangalia, aende katika sheria ya Bwana, Mungu wa Israeli, kwa moyo wake wote; hakutoka katika makosa ya Yeroboamu, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli. |
32. | Siku zile Bwana akaanza kupunguza Israeli. Hazaeli akawapiga mipakani mwote mwa Israeli; |
33. | kutoka Yordani upande wa mashariki, nchi yote ya Gileadi, na ya Wagadi, na Wareubeni, na Wamanase, kutoka Aroeri iliopo karibu na bonde la Arnoni, yaani, Gileadi, na Bashani. |
34. | Basi mambo yote ya Yehu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na ushujaa wake, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli? |
35. | Yehu akalala na babaze; wakamzika katika Samaria. Na Yehoahazi mwanawe akatawala mahali pake. |
36. | Na muda Yehu aliotawala juu ya Israeli katika Samaria ulikuwa miaka ishirini na minane. |
← 2Kings (10/25) → |