2Corinthians (1/13) → |
1. | Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo ndugu yetu; kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, pamoja na watakatifu wote walioko katika nchi yote ya Akaya. |
2. | Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo. |
3. | Na ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote; |
4. | atufarijiye katika dhiki zetu zote ili nasi tupate kuwafariji wale walio katika dhiki za namna zote, kwa faraja hizo, tunazofarijiwa na Mungu. |
5. | Kwa kuwa kama vile mateso ya Kristo yanavyozidi kwetu, vivyo hivyo faraja yetu inazidi kwa njia ya Kristo. |
6. | Lakini ikiwa sisi tu katika dhiki, ni kwa ajili ya faraja yenu na wokovu wenu; au ikiwa twafarijiwa, ni kwa ajili ya faraja yenu; ambayo hutenda kazi yake kwa kustahimili mateso yale yale tuteswayo na sisi. |
7. | Na tumaini letu kwa ajili yenu ni imara, tukijua ya kuwa kama vile mlivyo washiriki wa yale mateso, vivyo hivyo mmekuwa washiriki wa zile faraja. |
8. | Maana ndugu, hatupendi, msijue habari ya dhiki ile iliyotupata katika Asia, ya kwamba tulilemewa mno kuliko nguvu zetu, hata tukakata tamaa ya kuishi. |
9. | Naam, sisi wenyewe tulikuwa na hukumu ya mauti katika nafsi zetu ili tusijitumainie nafsi zetu, bali tumtumaini Mungu, awafufuaye wafu, |
10. | aliyetuokoa sisi katika mauti kuu namna ile; tena atatuokoa; ambaye tumemtumaini kwamba atazidi kutuokoa; |
11. | ninyi nanyi mkisaidiana nasi kwa ajili yetu katika kuomba, ili, kwa sababu ya ile karama tupewayo sisi kwa msaada wa watu wengi, watu wengi watoe shukrani kwa ajili yetu. |
12. | Kwa maana kujisifu kwetu ni huku, ushuhuda wa dhamiri yetu, ya kwamba kwa utakatifu na weupe wa moyo utokao kwa Mungu; si kwa hekima ya mwili, bali kwa neema ya Mungu; tulienenda katika dunia, na hasa kwenu ninyi. |
13. | Maana hatuwaandikii ninyi neno, ila yale msomayo, au kuyakiri; nami nataraji ya kuwa mtayakiri hayo hata mwisho; |
14. | vile vile kama mlivyotukiri kwa sehemu, ya kwamba sisi tu sababu ya kujisifu kwenu, kama ninyi mlivyo kwetu sisi, katika siku ile ya Bwana wetu Yesu. |
15. | Nami nikiwa na tumaini hilo nalitaka kufika kwenu hapo kwanza, ili mpate karama ya pili; |
16. | na kupita kwenu na kuendelea mpaka Makedonia; na tena toka Makedonia kurudi kwenu na kusafirishwa nanyi kwenda Uyahudi. |
17. | Basi, nilipokusudia hayo, je! Nalitumia kigeugeu? Au hayo niyakusudiayo, nayakusudia kwa jinsi ya mwili kwamba iwe hivi kwangu, kusema Ndiyo, ndiyo, na Siyo, siyo? |
18. | Lakini kama Mungu alivyo mwaminifu, neno letu kwenu si Ndiyo na siyo. |
19. | Maana Mwana wa Mungu, Kristo Yesu, aliyehubiriwa katikati yenu na sisi, yaani, mimi na Silwano na Timotheo, hakuwa Ndiyo na siyo; bali katika yeye ni Ndiyo. |
20. | Maana ahadi zote za Mungu zilizopo katika yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye ni Amin; Mungu apate kutukuzwa kwa sisi. |
21. | Basi Yeye atufanyaye imara pamoja nanyi katika Kristo, na kututia mafuta, ni Mungu, |
22. | naye ndiye aliyetutia muhuri akatupa arabuni ya Roho mioyoni mwetu. |
23. | Lakini mimi namwita Mungu awe shahidi juu ya roho yangu, ya kwamba, kwa kuwahurumia sijafika Korintho. |
24. | Si kwamba tunatawala imani yenu; bali tu wasaidizi wa furaha yenu; maana kwa imani yenu mnasimama. |
2Corinthians (1/13) → |