← 1Timothy (4/6) → |
1. | Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani; |
2. | kwa unafiki wa watu wasemao uongo, wakichomwa moto dhamiri zao wenyewe; |
3. | wakiwazuia watu wasioe, na kuwaamuru wajiepushe na vyakula, ambavyo Mungu aliviumba vipokewe kwa shukrani na walio na imani wenye kuijua hiyo kweli. |
4. | Kwa maana kila kiumbe cha Mungu ni kizuri, wala hakuna cha kukataliwa, kama kikipokewa kwa shukrani; |
5. | kwa kuwa kimetakaswa kwa neno la Mungu na kwa kuomba. |
6. | Uwakumbushe ndugu mambo hayo, nawe utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu, na mzoevu wa maneno ya imani, na mafundisho mazuri yale uliyoyafuata. |
7. | Bali hadithi za kizee, zisizokuwa za dini, uzikatae; nawe ujizoeze kupata utauwa. |
8. | Kwa maana kujizoeza kupata nguvu za mwili kwafaa kidogo, lakini utauwa hufaa kwa mambo yote; yaani, unayo ahadi ya uzima wa sasa, na ya ule utakaokuwapo baadaye. |
9. | Ni neno la kuaminiwa, tena lastahili kukubalika kabisa; |
10. | kwa maana twajitaabisha na kujitahidi kwa kusudi hili, kwa sababu tunamtumaini Mungu aliye hai, aliye Mwokozi wa watu wote, hasa wa waaminio. |
11. | Mambo hayo uyaagize na kuyafundisha. |
12. | Mtu awaye yote asiudharau ujana wako, bali uwe kielelezo kwao waaminio, katika usemi na mwenendo, na katika upendo na imani na usafi. |
13. | Hata nitakapokuja, ufanye bidii katika kusoma na kuonya na kufundisha. |
14. | Usiache kuitumia karama ile iliyomo ndani yako, uliyopewa kwa unabii na kwa kuwekewa mikono ya wazee. |
15. | Uyatafakari hayo; ukae katika hayo; ili kuendelea kwako kuwe dhahiri kwa watu wote. |
16. | Jitunze nafsi yako, na mafundisho yako. Dumu katika mambo hayo; maana kwa kufanya hivyo utajiokoa nafsi yako na wale wakusikiao pia. |
← 1Timothy (4/6) → |