← 1Thessalonians (4/5) → |
1. | Iliyobaki, ndugu, tunakusihini na kuwaonya kwamba mwenende katika Bwana Yesu; kama mlivyopokea kwetu jinsi iwapasavyo kuenenda na kumpendeza Mungu, kama nanyi mnavyoenenda, vivyo hivyo mpate kuzidi sana. |
2. | Kwa kuwa mnajua ni maagizo gani tuliyowapa kwa Bwana Yesu. |
3. | Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati; |
4. | kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima; |
5. | si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua Mungu. |
6. | Mtu asimpunje ndugu yake wala kumkosa katika jambo hili; kwa sababu Bwana ndiye alipizaye kisasi cha haya yote; kama tulivyowaambia kwanza, tukashuhudia sana. |
7. | Maana Mungu hakutuitia uchafu, bali tuwe katika utakaso. |
8. | Basi yeye anayekataa, hakatai mwanadamu bali Mungu, anayewapa ninyi Roho wake Mtakatifu. |
9. | Katika habari ya upendano, hamna haja niwaandikie; maana ninyi wenyewe mmefundishwa na Mungu kupendana. |
10. | Kwa maana mnafanya neno hili kwa ndugu wote walio katika Makedonia yote. Lakini twawasihi, ndugu, mzidi sana. |
11. | Tena mjitahidi kutulia, na kutenda shughuli zenu, na kufanya kazi kwa mikono yenu wenyewe, kama tulivyowaagiza; |
12. | ili mwenende kwa adabu mbele yao walio nje, wala msiwe na haja ya kitu cho chote. |
13. | Lakini, ndugu, hatutaki msijue habari zao waliolala mauti, msije mkahuzunika kama na wengine wasio na matumaini. |
14. | Maana, ikiwa twaamini ya kwamba Yesu alikufa akafufuka, vivyo hivyo na hao waliolala katika Yesu, Mungu atawaleta pamoja naye. |
15. | Kwa kuwa twawaambieni haya kwa neno la Bwana, kwamba sisi tulio hai, tutakaosalia hata wakati wa kuja kwake Bwana, hakika hatutawatangulia wao waliokwisha kulala mauti. |
16. | Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na mwaliko, na sauti ya malaika mkuu, na parapanda ya Mungu; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. |
17. | Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. |
18. | Basi, farijianeni kwa maneno hayo. |
← 1Thessalonians (4/5) → |