← 1Kings (5/22) → |
1. | Ndipo Hiramu, mfalme wa Tiro, akawatuma watumishi wake kwa Sulemani; kwani alikuwa amesikia ya kwamba wamemtia mafuta awe mfalme mahali pa baba yake. Kwa maana Hiramu alikuwa akimpenda Daudi siku zote. |
2. | Basi Sulemani akatuma watu kwa Hiramu, akasema, |
3. | Umemjua Daudi baba yangu jinsi asivyoweza kujenga nyumba kwa jina la Bwana, Mungu wake, kwa sababu ya vita vilivyomzunguka pande zote, hata Bwana alipowatia watu chini ya nyayo zake. |
4. | Ila leo Bwana, Mungu wangu, amenipa amani kila upande; hakuna adui, wala tukio baya. |
5. | Nami, tazama, nakusudia kujenga nyumba kwa jina la Bwana, Mungu wangu, kama Bwana alivyomwambia Daudi baba yangu, akisema, Mwana wako, nitakayemweka katika kiti chake cha enzi mahali pako, ndiye atakayeijenga nyumba kwa jina langu. |
6. | Basi uamuru wanikatie mierezi ya Lebanoni; na watumishi wangu watafuatana na watumishi wako; na ujira wa watumishi wako nitakupa kama utakavyosema; kwa kuwa wajua ya kwamba hakuna kwetu mtu ajuaye kukata miti kama Wasidoni. |
7. | Ikawa, Hiramu aliposikia maneno yake Sulemani, alifurahi sana, akasema, Na ahimidiwe Bwana leo, aliyempa Daudi mwana mwenye akili juu ya watu hawa walio wengi. |
8. | Hiramu akatuma watu kwa Sulemani, akasema, Nimeyasikia yale uliyoniletea; nami nitafanya kila ulitakalo katika habari ya miti ya mierezi, na miti ya miberoshi. |
9. | Watumishi wangu wataishusha toka Lebanoni mpaka baharini; nami nitaiendesha baharini, ikifungwa pamoja, mpaka mahali utakaponiagiza, huko nitaifungua ili wewe uichukue; ndivyo utakavyoitimiza haja yangu, ukiwapa chakula watu wa nyumbani mwangu. |
10. | Basi Hiramu akampa Sulemani miti ya mierezi na miti ya miberoshi kadiri alivyotaka. |
11. | Sulemani akampa Hiramu kori ishirini elfu za ngano, chakula cha watu wake, na kori ishirini za mafuta safi. Ndizo Sulemani alizompa Hiramu mwaka kwa mwaka. |
12. | Bwana akampa Sulemani hekima, kama alivyomwahidia. Ikawa amani kati yao Hiramu na Sulemani; wakafanyana maagano pamoja hao wawili. |
13. | Mfalme Sulemani akafanya shokoa ya Israeli wote; nayo shokoa hiyo ilikuwa ya watu thelathini elfu. |
14. | Akawatuma Lebanoni kwa mwezi, elfu kumi kwa zamu. Mwezi mmoja walikuwako huko Lebanoni, na miezi miwili wakawako kwao. Na Adoramu alikuwa juu ya shokoa. |
15. | Sulemani alikuwa na wachukua mizigo sabini elfu, na wakatao miti themanini elfu milimani; |
16. | mbali na maakida yake Sulemani waliokuwa juu ya kazi, elfu tatu na mia tatu, wasimamizi wa watu waliotenda kazi. |
17. | Mfalme akaamuru, nao wakaleta mawe makubwa, mawe ya thamani, ili wauweke msingi wa nyumba kwa mawe yaliyochongwa. |
18. | Na waashi wa Sulemani na waashi wa Hiramu na Wagebali wakayachonga, wakaweka tayari miti na mawe ya kuijenga nyumba. |
← 1Kings (5/22) → |