← 1Kings (12/22) → |
1. | Rehoboamu akaenda Shekemu; maana Israeli wote walikuwa wamekwenda Shekemu, ili kumfanya mfalme. |
2. | Ikawa Yeroboamu mwana wa Nebati alipopata habari (maana alikuwa akaliko Misri, huko alikokimbilia awe mbali na mfalme Sulemani; Yeroboamu akakaa huko Misri, |
3. | wakapeleka watu kwenda kumwita); basi Yeroboamu na jamii yote ya Israeli wakaenda, wakamwambia Rehoboamu, wakasema, |
4. | Baba yako alilifanya zito kongwa letu; basi sasa utupunguzie utumwa mzito tuliotumikishwa na baba yako, na lile kongwa zito alilotutwika, nasi tutakutumikia. |
5. | Akawaambia, Enendeni zenu hata siku ya tatu, kisha mnirudie tena. Watu wakaenda zao. |
6. | Mfalme Rehoboamu akataka shauri kwa wazee waliokuwa wakisimama mbele ya Sulemani, baba yake, alipokuwa hai, akasema, Mwanipa shauri gani ili niwajibu watu hawa? |
7. | Wakamwambia wakasema, Ukikubali kuwa mtumishi wa watu hawa leo, na kuwatumikia, na kuwajibu, na kuwapa maneno mazuri, basi watakuwa watumishi wako daima. |
8. | Lakini akaliacha shauri lile la wazee, walilompa, akataka shauri kwa wale vijana waliokua pamoja naye, na kusimama mbele yake. |
9. | Akawaambia, Mwanipa shauri gani ili tuwajibu watu hawa, waliosema nami, wakinena Utufanyie jepesi kongwa lile alilotutwika baba yako? |
10. | Na wale vijana waliokua pamoja naye wakamwambia, wakasema, Uwaambie hivi watu wale waliokuambia, wakisema, Baba yako alilifanya zito kongwa letu, bali wewe utufanyie jepesi, uwaambie hivi, Kidole changu cha mwisho ni kinene kuliko kiuno cha baba yangu. |
11. | Basi kama vile baba yangu alivyowatwika kongwa zito, mimi nitaongeza kongwa lenu; baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, bali mimi nitawapigeni kwa nge. |
12. | Basi, Yeroboamu na watu wote wakamfikia Rehoboamu siku ya tatu, kama mfalme alivyoamuru, akisema, Mnirudie siku ya tatu. |
13. | Mfalme akawajibu watu wale kwa ukali, akaliacha shauri lile wazee walilompa; |
14. | akawajibu kama vile walivyomshauri vijana, akasema, Baba yangu alilifanya zito kongwa lenu, bali mimi nitaongeza kongwa lenu; baba yangu aliwapiga kwa mijeledi, bali mimi nitawapigeni kwa nge. |
15. | Basi mfalme hakuwasikia wale watu; maana jambo hili lilitoka kwa Bwana, ili alitimize neno lake, Bwana alilomwambia Yeroboamu mwana wa Nebati kwa kinywa cha Ahiya Mshiloni. |
16. | Basi Israeli wote walipoona ya kuwa mfalme hakuwasikia, hao watu walimjibu mfalme, wakasema, Tuna sehemu gani katika Daudi? Wala hatuna urithi katika mwana wa Yese. Haya! Nendeni zenu hemani kwenu, enyi Israeli; sasa itunze nyumba yako mwenyewe, Ee Daudi. Hivyo Israeli wakaenda zao hemani kwao. |
17. | Lakini kwa habari za wana wa Israeli waliokaa katika miji ya Yuda, Rehoboamu aliwatawala wao. |
18. | Ndipo mfalme Rehoboamu akampeleka Adoramu, aliyekuwa juu ya shokoa, nao Israeli wote wakampiga kwa mawe hata akafa. Mfalme Rehoboamu akafanya haraka kupanda katika gari, ili akimbilie Yerusalemu. |
19. | Hivyo Israeli wakaasi juu ya nyumba ya Daudi hata leo. |
20. | Ikawa, Israeli wote waliposikia ya kwamba Yeroboamu amerudi, wakapeleka watu wakamwita aje mkutanoni, wakamfanya mfalme juu ya Israeli wote; wala hapakuwa na mtu aliyeshikamana na nyumba ya Daudi, ila kabila ya Yuda peke yake. |
21. | Hata Rehoboamu alipofika Yerusalemu, akakusanya nyumba yote ya Yuda, pamoja na kabila ya Benyamini, watu wateule mia na themanini elfu, waliokuwa watu wa vita, ili wapigane na nyumba ya Israeli, waurudishe ufalme tena kwa Rehoboamu mwana wa Sulemani. |
22. | Lakini likaja neno la Mungu kwa Shemaya mtu wa Mungu, kusema, |
23. | Mwambie Rehoboamu mwana wa Sulemani, mfalme wa Yuda, na jamaa yote ya Yuda na Benyamini, na watu waliosalia, ukisema, |
24. | Bwana asema hivi, Msiende, wala msipigane na ndugu zenu wana wa Israeli; rudini kila mtu nyumbani kwake; kwa kuwa jambo hili limetoka kwangu. Basi, wakalisikiliza neno la Bwana, wakarudi, wakaenda zao, sawasawa na neno la Bwana. |
25. | Ndipo Yeroboamu akajenga Shekemu katika milima ya Efraimu, akakaa huko. Akatoka huko akajenga Penueli. |
26. | Yeroboamu akasema moyoni mwake, Basi ufalme utairudia nyumba ya Daudi. |
27. | Kama watu hawa wakipanda kwenda kutoa dhabihu katika nyumba ya Bwana huko Yerusalemu, ndipo mioyo ya watu hawa itamrudia bwana wao, yaani Rehoboamu, mfalme wa Yuda; nao wataniua mimi, na kumrudia Rehoboamu, mfalme wa Yuda. |
28. | Kwa hiyo mfalme akafanya shauri, akafanyiza ng'ombe wawili wa dhahabu, akawaambia watu, Ni vigumu kwenu kupanda kwenda Yerusalemu; tazama, hii ndiyo miungu yenu, enyi Israeli, iliyowapandisha kutoka nchi ya Misri. |
29. | Akamweka mmoja katika Betheli, na wa pili akamweka katika Dani. |
30. | Jambo hili likawa dhambi, maana watu walikwenda kuabudu mbele ya kila mmoja, hata huko Dani. |
31. | Tena akafanya nyumba za mahali pa juu, akafanya na watu wo wote, watu wasio wa wana wa Lawi, kuwa makuhani. |
32. | Yeroboamu akaamuru kushika sikukuu katika mwezi wa nane, siku ya kumi na tano ya mwezi, mfano wa sikukuu iliyokuwa katika Yuda, akapanda juu ili kuiendea madhabahu. Akafanya vivyo katika Betheli akiwatolea dhabihu wale ng'ombe aliowafanya; akawaweka katika Betheli wale makuhani wa mahali pa juu alipokuwa amepafanya. |
33. | Akatoa dhabihu juu ya ile madhabahu aliyoifanya katika Betheli, siku ya kumi na tano ya mwezi wa nane, mwezi aliouwaza moyoni mwake mwenyewe; akawaamuru wana wa Israeli waishike sikukuu hiyo, akapanda kuiendea madhabahu, ili kufukiza uvumba. |
← 1Kings (12/22) → |