← 1Kings (10/22) → |
1. | Na malkia wa Sheba aliposikia habari za Sulemani juu ya jina la Bwana, alikuja ili amjaribu kwa maswali ya fumbo. |
2. | Akaingia Yerusalemu na wafuasi wengi sana, na ngamia wachukuao manukato, na dhahabu nyingi sana, na vito vya thamani; alipomfikilia Sulemani, akazungumza naye mambo yote aliyokuwa nayo moyoni. |
3. | Naye Sulemani akamfumbulia maswali yake yote; wala hakukuwa na neno alilofichiwa mfalme asimwambie. |
4. | Naye malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Sulemani, na nyumba aliyokuwa ameijenga, |
5. | na chakula cha mezani pake, na watumishi wake walivyokaa, na kusimamia kwao wangoje wake, na mavazi yao, na wanyweshaji wake, na daraja yake ya kupandia mpaka nyumba ya Bwana, roho yake ilizimia. |
6. | Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako. |
7. | Lakini mimi sikuzisadiki habari hizo, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; tena, tazama, sikuambiwa nusu; wewe umezidi kwa hekima na kufanikiwa kuliko habari nilizozisikia. |
8. | Heri watu wako, na heri watumishi hawa wako, wasimamao mbele yako siku zote, wakisikia hekima yako. |
9. | Na ahimidiwe Bwana, Mungu wako, aliyependezwa nawe, ili akuweke juu ya kiti cha enzi cha Israeli; kwa kuwa Bwana amewapenda Israeli milele, kwa hiyo amekufanya kuwa mfalme, ufanye hukumu na haki. |
10. | Basi akampa mfalme talanta za dhahabu mia na ishirini, na manukato mengi, mengi sana, na vito vya thamani; wala haukuja tena wingi wa manukato, kama hayo malkia wa Sheba aliyompa mfalme Sulemani. |
11. | Tena merikebu za Hiramu, zilizochukua dhahabu kutoka Ofiri, zikaleta kutoka Ofiri miti ya msandali mingi sana, na vito vya thamani. |
12. | Mfalme akafanya kwa mia hiyo ya msandali nguzo za nyumba ya Bwana, na za nyumba ya mfalme, na vinubi na vinanda vya hao waimbaji; wala haikuja miti ya msandali kama hiyo, wala haikuonekana, hata leo. |
13. | Naye mfalme Sulemani akampa malkia wa Sheba haja yake yote, kila alilotaka, zaidi ya hayo aliyopewa na Sulemani kwa ukarimu wake wa kifalme. Basi, akarudi akaenda zake katika nchi yake, yeye na watumishi wake. |
14. | Basi uzani wa dhahabu iliyomfikia Sulemani mwaka mmoja, ndio talanta mia sita sitini na sita, |
15. | zaidi ya faida ya wachuuzi, na bidhaa ya wafanya biashara, na ya wafalme wote wa hao waliochanganyika, na ya maliwali wa nchi. |
16. | Mfalme Sulemani akafanya ngao mia mbili za dhahabu iliyofuliwa; kila ngao moja ilipata shekeli mia sita za dhahabu. |
17. | Na vigao mia tatu vya dhahabu iliyofuliwa; kila kigao kimoja kilipata mane tatu za dhahabu. Mfalme akaviweka katika nyumba ya mwitu wa Lebanoni. |
18. | Tena mfalme akafanya kiti cha enzi kikubwa cha pembe, akakifunikiza kwa dhahabu iliyo safi. |
19. | Kiti kile kilikuwa na daraja sita, na juu yake kimeviringana nyuma; na mikono huko na huko mahali pa kuketi, na simba wawili wakisimama kando ya hiyo mikono. |
20. | Na simba kumi na wawili wamesimama juu ya daraja sita huko na huko; wala hakikufanyika kwa mkono wake katika ufalme wo wote. |
21. | Na vyombo vyote vya kunywea vya mfalme Sulemani vilikuwa vya dhahabu, na vyombo vyote vya nyumba ya mwitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu iliyosafika; hakuna vya fedha, fedha haikuhesabiwa kuwa kitu siku za Sulemani. |
22. | Kwa kuwa mfalme alikuwa na merikebu za Tarshishi baharini pamoja na merikebu za Hiramu; mara moja katika miaka mitatu huja merikebu za Tarshishi, zikileta dhahabu, na fedha, na pembe, na nyani, na tausi. |
23. | Basi mfalme Sulemani akawapita wafalme wote wa duniani kwa mali, na kwa hekima. |
24. | Ulimwengu wote ukamtafuta Sulemani uso wake, ili waisikie hekima yake, Mungu aliyomtia moyoni. |
25. | Wakaleta kila mtu zawadi yake, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi, na silaha, na manukato, na farasi, na nyumbu, hesabu yake ya mwaka kwa mwaka. |
26. | Sulemani akakusanya magari na wapandao farasi; naye alikuwa na magari elfu na mia nne, na wapandao farasi kumi na mbili elfu, aliowaweka katika miji ya magari, na pamoja na mfalme huko Yerusalemu. |
27. | Mfalme akafanya fedha humo Yerusalemu kuwa kama mawe, na mierezi akaifinya kuwa kama mikuyu iliyomo Shefela, kwa kuwa mingi. |
28. | Nao farasi aliokuwa nao Sulemani wakaletwa toka Misri; wakapewa wafanya biashara wake mfalme kwa makundi, kila kundi na thamani yake. |
29. | Tena gari huja kutoka katika Misri kwa shekeli mia sita za fedha, na farasi mmoja kwa mia hamsini; vivyo watu wakawaletea wafalme wote wa Wahiti, na wafalme wa Shamu, mikononi mwao. |
← 1Kings (10/22) → |