| ← 1Corinthians (6/16) → |
| 1. | Je! Mtu wa kwenu akiwa ana daawa juu ya mwenzake athubutu kushitaki mbele ya wasio haki, wala si mbele ya watakatifu? |
| 2. | Au hamjui ya kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Na ikiwa ulimwengu utahukumiwa na ninyi, je! Hamstahili kukata hukumu zilizo ndogo? |
| 3. | Hamjui ya kuwa mtawahukumu malaika, basi si zaidi sana mambo ya maisha haya? |
| 4. | Basi, mkiwa na mahali panapohukumiwa mambo ya maisha haya, mwawaweka kuwa waamuzi hao waliohesabiwa kuwa si kitu; katika kanisa? |
| 5. | Nasema hayo nipate kuwatahayarisha. Je! Ndivyo, kwamba kwenu hakuna hata mtu mmoja mwenye hekima, awezaye kukata maneno ya ndugu zake? |
| 6. | Bali mwashitakiana, ndugu kwa ndugu, tena mbele yao wasioamini. |
| 7. | Basi imekuwa upungufu kwenu kabisa kwamba mnashitakiana ninyi kwa ninyi. Maana si afadhali kudhulumiwa? Maana si afadhali kunyang'anywa mali zenu? |
| 8. | Bali kinyume cha hayo ninyi wenyewe mwadhulumu watu na kunyang'anya mali zao; naam, hata za ndugu zenu. |
| 9. | Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa Mungu? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa Mungu, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti, |
| 10. | wala wevi, wala watamanio, wala walevi, wala watukanaji, wala wanyang'anyi. |
| 11. | Na baadhi yenu mlikuwa watu wa namna hii; lakini mlioshwa, lakini mlitakaswa, lakini mlihesabiwa haki katika jina la Bwana Yesu Kristo, na katika Roho wa Mungu wetu. |
| 12. | Vitu vyote ni halali kwangu, lakini si vyote vifaavyo; vitu vyote ni halali kwangu, lakini mimi sitatiwa chini ya uwezo wa kitu cho chote. |
| 13. | Vyakula ni kwa tumbo, na tumbo ni kwa vyakula; lakini Mungu atavitowesha vyote viwili, tumbo na vyakula. Lakini mwili si kwa zinaa, bali ni kwa Bwana, naye Bwana ni kwa mwili. |
| 14. | Naye Mungu alimfufua Bwana, na tena atatufufua sisi kwa uweza wake. |
| 15. | Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba? Hasha! |
| 16. | Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja. |
| 17. | Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye. |
| 18. | Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe. |
| 19. | Au hamjui ya kuwa mwili wenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Wala ninyi si mali yenu wenyewe; |
| 20. | maana mlinunuliwa kwa thamani. Sasa basi, mtukuzeni Mungu katika miili yenu. |
| ← 1Corinthians (6/16) → |