← 1Chronicles (22/29) → |
1. | Ndipo Daudi akasema, Hii ndiyo nyumba ya Bwana Mungu, na hii ndiyo madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa kwa Israeli. |
2. | Basi Daudi akaamuru wakusanyike wageni waliokuwa katika nchi ya Israeli; akaweka waashi wachonge mawe ili kujenga nyumba ya Mungu. |
3. | Daudi akaweka akiba tele ya chuma kwa misumari ya tarabe za malango, na kwa mafungo; na ya shaba akiba tele isiyo na uzani; |
4. | na mierezi isiyo na idadi; kwa kuwa Wasidoni na watu wa Tiro wakamletea Daudi mierezi tele. |
5. | Daudi akasema, Sulemani mwanangu akali ni mchanga bado, na mwororo, nayo nyumba atakayojengewa Bwana haina budi kuwa nzuri mno, yenye sifa na yenye fahari katika nchi zote; kwa hiyo mimi nitaiwekea akiba. Basi Daudi akaweka akiba tele kabla hajafa. |
6. | Ndipo akamwita Sulemani mwanawe, akamwagiza amjengee Bwana, Mungu wa Israeli, nyumba. |
7. | Daudi akamwambia Sulemani mwanawe, Kwangu mimi nia yangu ilikuwa kujenga nyumba kwa ajili ya jina la Bwana, Mungu wangu. |
8. | Lakini neno la Bwana likanijia, kusema, Wewe umemwaga damu nyingi, na vita vikubwa umevifanya; wewe hutajenga nyumba kwa ajili ya jina langu, kwa sababu umemwaga damu nyingi juu ya nchi machoni pangu; |
9. | tazama, utazaliwa mwana, atakayekuwa mtu wa kustarehe; nami nitamstarehesha mbele ya adui zake pande zote; kwani jina lake litakuwa Sulemani, |
10. | huyo ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya jina langu; naye atakuwa mwanangu, nami nitakuwa babaye; nami nitakifanya imara milele kiti cha ufalme wake juu ya Israeli. |
11. | Sasa mwanangu, Bwana na awe pamoja nawe; ukafanikiwe, na kuijenga nyumba ya Bwana, Mungu wako, kama alivyonena kwa habari zako. |
12. | Bwana na akupe busara na akili, akakuagizie juu ya Israeli; ili uishike torati ya Bwana, Mungu wako. |
13. | Ndipo utakapofanikiwa, ukiangalia kuzitenda amri, na hukumu, Bwana alizomwagizia Musa juu ya Israeli; uwe hodari, na wa moyo mkuu; usiogope wala usifadhaike. |
14. | Basi sasa, tazama, katika shida yangu, nimeiwekea akiba nyumba ya Bwana, talanta elfu mia za dhahabu, na talanta elfu elfu za fedha; na shaba na chuma isiyo na uzani; kwa vile zilivyo tele; miti tena na mawe nimeweka akiba, nawe utaweza kuongeza. |
15. | Tena kwako kuna mafundi wengi, wenye kuchonga na kufanyiza kazi ya mawe na miti, na kila aliye mstadi kwa kazi yo yote; |
16. | ya dhahabu, ya fedha, na ya shaba, na ya chuma, hapana hesabu; basi inuka ushike kazi, naye Bwana na awe pamoja nawe. |
17. | Tena Daudi akawaamuru wakuu wote wa Israeli, kwamba wamsaidie Sulemani mwanawe, akisema, |
18. | Je! Si Bwana, Mungu wenu, aliye pamoja nanyi? Na kuwastarehesha pande zote? Kwa kuwa wenyeji wa nchi amewatia mkononi mwangu; nayo nchi imetiishwa mbele za Bwana, na mbele ya watu wake. |
19. | Basi sasa jitieni moyo na nia kumtafuta Bwana, Mungu wenu; inukeni basi, mkamjengee Bwana Mungu mahali patakatifu, ili kulileta sanduku la agano la Bwana, na vyombo vitakatifu vya Mungu, ndani ya nyumba itakayojengwa kwa ajili ya jina la Bwana. |
← 1Chronicles (22/29) → |