← 1Chronicles (18/29) → |
1. | Ikawa baadaye, Daudi akawapiga Wafilisti, akawashinda, akautwaa Gathi na vijiji vyake mikononi mwa Wafilisti. |
2. | Akapiga Moabu; na hao Wamoabi wakawa watumwa wa Daudi wakaleta zawadi. |
3. | Tena Daudi akampiga Hadadezeri, mfalme wa Soba, mpaka Hamathi, alipokwenda kujisimamishia mamlaka yake kwenye mto wa Frati. |
4. | Daudi akampokonya magari elfu, na wapanda farasi saba elfu, na askari waendao kwa miguu ishirini elfu; Daudi akawakata mshipa farasi wote wa magari, ila wa magari mia akawaweka. |
5. | Na Washami wa Dameski walipokuja wamsaidie Hadadezeri, mfalme wa Soba, Daudi akapiga katika hao Washami watu ishirini na mbili elfu. |
6. | Ndipo Daudi akaweka ngome katika Shamu ya Dameski; nao Washami wakawa watumwa wa Daudi, wakaleta zawadi. Naye Bwana akampa Daudi kushinda kila alikokwenda. |
7. | Tena Daudi akazitwaa ngao za dhahabu zilizovaliwa na watumishi wa Hadadezeri akazileta Yerusalemu. |
8. | Tena toka Tibhathi, na toka Berothai, miji ya Hadadezeri, Daudi akatwaa shaba nyingi mno, aliyofanyizia Sulemani ile bahari ya shaba, na zile nguzo, na vile vyombo vya shaba. |
9. | Hata aliposikia Tou, mfalme wa Hamathi, ya kuwa Daudi amewapiga jeshi lote la Hadadezeri, mfalme wa Soba, |
10. | akampeleka mwanawe Hadoramu kwa mfalme Daudi, ili kumsalimia, na kumbarikia, kwa sababu alikuwa amepigana na Hadadezeri, na kumpiga; kwa maana Hadadezeri alikuwa amepigana vita juu ya Tou; naye akaleta vyombo vya dhahabu, na fedha, na shaba, vya namna zote. |
11. | Hivi pia mfalme Daudi akavifanya wakfu kwa Bwana, pamoja na hiyo fedha na dhahabu, aliyoteka nyara kwa mataifa yote; kwa Edomu, na kwa Moabu, na kwa wana wa Amoni, na kwa Wafilisti, na kwa Amaleki. |
12. | Tena Abishai, mwana wa Seruya, akawapiga wa Waedomi katika Bonde la Chumvi watu kumi na nane elfu. |
13. | Akaweka ngome katika Edomu; na Waedomi wote wakawa watumwa wa Daudi. Naye Bwana akampa Daudi kushinda, kila alikokwenda. |
14. | Basi Daudi akatawala juu ya Israeli wote; akawafanyia hukumu na haki watu wake wote. |
15. | Na Yoabu mwana wa Seruya akawa juu ya jeshi; na Yehoshafati mwana wa Ahiludi mwenye kuandika tarehe. |
16. | Na Sadoki mwana wa Ahitubu, na Ahimeleki mwana wa Abiathari, walikuwa makuhani; na Shausha mwandishi; |
17. | na Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa juu ya Wakerethi na Wapelethi; na wana wa Daudi walikuwa wakuu kumzunguka mfalme. |
← 1Chronicles (18/29) → |