← 1Chronicles (15/29) → |
1. | Basi Daudi akajifanyia nyumba katika mji wa Daudi; akapaweka tayari mahali kwa ajili ya sanduku la Mungu, akalipigia hema. |
2. | Ndipo Daudi akasema, Haimpasi mtu awaye yote kulichukua sanduku la Mungu, isipokuwa Walawi peke yao; kwa kuwa hao ndio aliowachagua Bwana, ili walichukue sanduku la Mungu, na kumtumikia daima. |
3. | Basi Daudi akawakusanya Israeli wote huko Yerusalemu, ili kulipandisha sanduku la Bwana, mpaka mahali pake alipoliwekea tayari. |
4. | Daudi akawakutanisha wana wa Haruni, na Walawi; |
5. | wa wana wa Kohathi; Urieli mkuu wao, na nduguze mia na ishirini; |
6. | wa wana wa Merari; Asaya mkuu wao, na nduguze mia mbili na ishirini; |
7. | wa wana wa Gershoni; Yoeli mkuu wao, na nduguze mia na thelathini; |
8. | wa wana wa Elsafani; Shemaya mkuu wao, na nduguze mia mbili; |
9. | wa wana wa Hebroni; Elieli mkuu wao, na nduguze themanini; |
10. | wa wana wa Uzieli; Aminadabu mkuu wao, na nduguze mia na kumi na wawili. |
11. | Tena, Daudi akawaita Sadoki na Abiathari makuhani, na hao Walawi, Urieli, Asaya, Yoeli, Shemaya, Elieli, na Aminadabu, |
12. | akawaambia, Ninyi ni vichwa vya mbari za baba za Walawi; jitakaseni, ninyi na ndugu zenu, ili mlipandishe sanduku la Bwana, Mungu wa Israeli, mpaka mahali pale nilipoliwekea tayari. |
13. | Kwani kwa sababu ninyi hamkulichukua safari ya kwanza, Bwana, Mungu wetu, alitufurikia, kwa maana hatukumtafuta sawasawa na sheria. |
14. | Basi makuhani na Walawi wakajitakasa, ili wapate kulipandisha sanduku la Bwana, Mungu wa Israeli. |
15. | Na wana wa Walawi wakalichukua sanduku la Mungu mabegani mwao kwa miti yake, kama vile Musa alivyoamuru, sawasawa na neno la Bwana. |
16. | Kisha Daudi akamwambia mkuu wa Walawi, kwamba awaagize ndugu zao waimbaji, pamoja na vyombo vyao vya kupigia ngoma, vinanda, na vinubi, na matoazi, wavipige na kupaza sauti kwa furaha. |
17. | Basi Walawi wakamwagiza Hemani mwana wa Yoeli; na wa nduguze, Asafu mwana wa Berekia; na wa wana wa Merari ndugu zao, Ethani mwana wa Kishi; |
18. | na pamoja nao ndugu zao kwa cheo cha pili, Zekaria, na Yaasieli, na Shemiramothi, na Yehieli, na Uni, na Eliabu; na Benaya, na Maaseya, na Matithia, na Elifelehu, na Mikneya, na Obed-edomu, na Yeieli, mabawabu. |
19. | Hivyo hao waimbaji, Hemani, Asafu, na Ethani, wakaagizwa kupiga matoazi yao ya shaba kwa sauti kuu; |
20. | na Zekaria, na Yaasieli na Shemiramothi, na Yehieli, na Uni, na Eliabu, na Maaseya, na Benaya, wenye vinanda vya sauti ya Alamothi; |
21. | na Matithiya, na Elifelehu, na Mikneya, na Obed-edomu, na Yeieli, na Azazia, wenye vinubi vya sauti ya Sheminithi, |
22. | waongoze. Na Kenania, mkuu wa Walawi, alikuwa juu ya uchukuzi; yeye aliusimamia uchukuzi, kwa sababu alikuwa mstadi. |
23. | Na Berekia na Elkana walikuwa mabawabu kwa ajili ya sanduku. |
24. | Na Shebania, na Yoshafati, na Nethaneli, na Amasai, na Zekaria, na Benaya, na Eliezeri, makuhani, wakapiga baragumu mbele ya sanduku la Mungu; na Obed-edomu na Yehia walikuwa mabawabu kwa ajili ya sanduku. |
25. | Basi Daudi, na wazee wa Israeli, na maakida wa maelfu, wakaenda, ili kulipandisha sanduku la agano la Bwana kutoka nyumbani mwa Obed-edomu kwa furaha kuu; |
26. | hata ikawa, Mungu alipowajalia Walawi waliolichukua sanduku la agano la Bwana, wakachinja ng'ombe saba, na kondoo waume saba. |
27. | Naye Daudi alikuwa amevaa joho ya kitani safi, na Walawi wote waliolichukua sanduku, na waimbaji, na Kenania msimamizi wa uchukuzi, na waimbaji; naye Daudi alikuwa amevaa naivera ya kitani. |
28. | Ndivyo Israeli wote walivyolipandisha sanduku la agano la Bwana kwa shangwe na kwa sauti ya tarumbeta, na kwa baragumu, na kwa matoazi, wakipiga sauti kuu kwa vinanda na vinubi. |
29. | Hata ikawa, sanduku la agano la Bwana lilipofika mjini kwa Daudi, Mikali binti Sauli akachungulia dirishani, akamwona mfalme Daudi, akicheza na kushangilia; akamdharau moyoni mwake. |
← 1Chronicles (15/29) → |