Zechariah (8/14)  

1. Neno la Bwana wa majeshi likanijia, kusema,
2. Bwana wa majeshi asema hivi, Mimi nina wivu kwa ajili ya Sayuni, wivu mkuu, nami nina wivu kwa ajili yake kwa ghadhabu kuu.
3. Bwana asema hivi, Mimi nimerudi Sayuni, nami nitakaa katikati ya Yerusalemu; na Yerusalemu utaitwa, Mji wa kweli; na Mlima wa Bwana wa majeshi utaitwa, Mlima mtakatifu.
4. Bwana wa majeshi asema hivi, Wazee wanaume na wazee wanawake watakaa tena katika njia za Yerusalemu, kila mtu ana mkongojo wake mkononi, kwa kuwa ni mzee sana.
5. Na hizo njia za mji zitajaa wavulana, na wasichana, wakicheza katika njia zake.
6. Bwana wa majeshi asema hivi, Ingawa hili ni neno lililo gumu mbele ya macho ya mabaki ya watu hawa katika siku hizo, je! Liwe neno gumu mbele ya macho yangu? Asema Bwana wa majeshi.
7. Bwana wa majeshi asema hivi, Tazama, nitawaokoa watu wangu toka nchi ya mashariki, na toka nchi ya magharibi;
8. nami nitawaleta, nao watakaa katikati ya Yerusalemu; nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao, katika kweli na katika haki.
9. Bwana wa majeshi asema hivi, Mikono yenu na iwe hodari, ninyi mnaosikia siku hizi maneno haya kwa vinywa vya manabii, waliokuwapo siku hiyo ulipowekwa msingi wa nyumba ya Bwana wa majeshi; yaani, hekalu hilo; ili lijengwe.
10. Maana kabla ya siku zile hapakuwa na ijara kwa mwanadamu, wala hapakuwa na ijara kwa mnyama; wala hapakuwa na amani kwake yeye aliyetoka, wala kwake yeye aliyeingia, kwa sababu ya adui; nami nalimwacha kila mtu kugombana na jirani yake.
11. Lakini sasa sitakuwa kwa mabaki ya watu hawa kama nilivyokuwa siku zile za kwanza, asema Bwana wa majeshi.
12. Kwa maana itakuwako mbegu ya amani; mzabibu utatoa matunda yake, nayo ardhi itatoa mazao yake, na hizo mbingu zitatoa umande wake; nami nitawarithisha mabaki ya watu hawa vitu hivi vyote.
13. Kisha itakuwa, kama vile mlivyokuwa laana katika mataifa, Ee nyumba ya Yuda, na nyumba ya Israeli, ndivyo nitakavyowaokoa, nanyi mtakuwa baraka; msiogope, lakini mikono yenu na iwe hodari.
14. Maana Bwana wa majeshi asema hivi, Kama vile nilivyoazimia kuwatenda ninyi mabaya, baba zenu waliponikasirisha, asema Bwana wa majeshi, wala mimi sikujuta;
15. vivyo hivyo nimeazimia katika siku hizi kuutendea Yerusalemu mema, na nyumba ya Yuda pia; msiogope.
16. Haya ndiyo mtakayoyatenda; kila mtu na aseme kweli na jirani yake; hukumuni kweli na hukumu ya amani malangoni mwenu;
17. wala mtu wa kwenu asiwaze mabaya moyoni mwake juu ya jirani yake; wala msipende kiapo cha uongo; maana hayo yote ndiyo niyachukiayo, asema Bwana.
18. Tena neno la Bwana wa majeshi likanijia, kusema,
19. Bwana wa majeshi asema hivi, Saumu ya mwezi wa nne, na saumu ya mwezi wa tano, na saumu ya mwezi wa saba, na saumu ya mwezi wa kumi, zitakuwa furaha na shangwe, na sikukuu za kuchangamkia, kwa nyumba ya Yuda; basi zipendeni kweli na amani.
20. Bwana wa majeshi asema hivi, Itatokea halafu ya kwamba watakuja mataifa na wenyeji wa miji mingi;
21. wenyeji wa mji huu watauendea mji huu, wakisema, Haya! Twendeni zetu kwa haraka tuombe fadhili za Bwana, na kumtafuta Bwana wa majeshi; Mimi nami nitakwenda.
22. Naam, watu wa kabila nyingi na mataifa hodari watakuja Yerusalemu kumtafuta Bwana wa majeshi, na kuomba fadhili za Bwana.
23. Bwana wa majeshi asema hivi, Siku hizo watu kumi, wa lugha zote za mataifa, wataushika upindo wa nguo yake yeye aliye Myahudi; naam, wataushika wakisema, Tutakwenda pamoja nanyi, kwa maana tumesikia kwamba Mungu yu pamoja nanyi.

  Zechariah (8/14)