← Zechariah (6/14) → |
1. | Nikainua macho yangu tena, nikaona, na tazama, yanatokea magari ya vita manne, yanatoka kati ya milima miwili, na milima hiyo ilikuwa ni milima ya shaba. |
2. | Katika gari la kwanza walikuwa farasi wekundu; na katika gari la pili walikuwa farasi weusi; |
3. | na katika gari la tatu walikuwa farasi weupe; na katika gari la nne walikuwa farasi wa rangi ya kijivujivu. |
4. | Nikajibu, nikamwuliza yule malaika aliyesema nami, Hawa ni nini, Bwana wangu? |
5. | Malaika akajibu, akaniambia, Hawa ni pepo nne za mbinguni, zitokeazo baada ya kusimama mbele za Bwana wa dunia yote. |
6. | Gari lile lenye farasi weusi latoka kwenda hata nchi ya kaskazini; nao farasi weupe wakatoka wakafuata nyuma yao; na wale wa rangi ya kijivujivu wakatoka kwenda hata nchi ya kusini. |
7. | Na wale wekundu wakatoka, wakataka kwenda huko na huko katika dunia; naye akawaambia, Haya! Tokeni, mwende huko na huko katika dunia. Basi wakaenda huko na huko katika dunia. |
8. | Ndipo akaniita, akaniambia akisema, Tazama, wale waendao mpaka nchi ya kaskazini wameituliza roho yangu katika nchi ya kaskazini. |
9. | Neno la Bwana likanijia, kusema, |
10. | Pokea vitu mikononi mwa baadhi ya watu waliohamishwa, yaani, Heldai, na Tobia, na Yedaya; na siku iyo hiyo enenda ukaingie katika nyumba ya Yosia, mwana wa Sefania, waliyoifikia kutoka Babeli; |
11. | naam, pokea fedha na dhahabu, ukafanye taji, ukamvike kichwani Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu; |
12. | ukamwambie, ukisema, Bwana wa majeshi asema hivi, ya kwamba, Tazama, mtu huyu ndiye ambaye jina lake ni Chipukizi; naye atakua katika mahali pake, naye atalijenga hekalu la Bwana. |
13. | Naam, yeye atalijenga hekalu la Bwana; naye atauchukua huo utukufu; ataketi akimiliki katika kiti chake cha enzi; na kutakuwa na kuhani katika kiti chake cha enzi; na shauri la amani litakuwa kati ya hao wawili. |
14. | Na hizo taji zitakuwa za Heldai, na Tobia, na Yedaya; na kwa fadhili za mwana wa Sefania; ziwe ukumbusho katika hekalu la Bwana. |
15. | Nao walio mbali watakuja na kujenga katika hekalu la Bwana, nanyi mtajua ya kuwa Bwana wa majeshi amenituma kwenu. Na haya yatatokea, kama mkijitahidi kuitii sauti ya Bwana, Mungu wenu. |
← Zechariah (6/14) → |