Zechariah (11/14)  

1. Ifungue milango yako, Ee Lebanoni, Ili moto uiteketeze mierezi yako.
2. Piga yowe, msunobari, maana mwerezi umeanguka, Kwa sababu miti iliyo mizuri imeharibika; Pigeni yowe, enyi mialoni ya Bashani, Kwa maana msitu wenye nguvu umeangamia.
3. Sauti ya wachungaji, ya uchungu mwingi! Kwa maana utukufu wao umeharibika; Sauti ya ngurumo ya wana-simba! Kwa maana kiburi cha Yordani kimeharibika.
4. Bwana, Mungu wangu, alisema hivi, Lilishe kundi la machinjo,
5. ambalo wenye kundi hilo huwachinja, kisha hujiona kuwa hawana hatia; na hao wawauzao husema, Na ahimidiwe Bwana, kwa maana mimi ni tajiri; na wachungaji wao wenyewe hawawahurumii.
6. Maana mimi sitawahurumia tena wenyeji wa nchi hii, asema Bwana; bali, tazama, nitawatia, kila mmoja wao, mikononi mwa mwenzake, na mikononi mwa mfalme; nao wataipiga hiyo nchi, wala mimi sitawaokoa mikononi mwao.
7. Basi nikalilisha kundi la machinjo, kweli kondoo waliokuwa wanyonge kabisa.
8. Nami nikawakatilia mbali wachungaji watatu katika mwezi mmoja; maana nafsi yangu ilikuwa imechoka kwa ajili yao, na nafsi zao pia walinichukia.
9. Ndipo nikasema, Sitawalisheni; afaye na afe; atakayekatiliwa mbali na akatiliwe mbali; nao waliosalia, kila mmoja na ale nyama ya mwili wa mwenziwe.
10. Nikaitwaa hiyo fimbo yangu, iitwayo Neema, nikaikata vipande viwili, ili nipate kulivunja agano langu nililolifanya na watu wa kabila zote.
11. Nayo ikavunjwa siku ile; na hivyo wale kondoo wanyonge walionisikiliza wakajua ya kuwa neno hili ndilo neno la Bwana.
12. Nikawaambia, Mkiona vema, nipeni ujira wangu; kama sivyo, msinipe. Basi wakanipimia vipande thelathini vya fedha, kuwa ndio ujira wangu.
13. Kisha Bwana akaniambia, Mtupie mfinyanzi kima kizuri, hicho nilichotiwa kima na watu hao. Basi nikavitwaa vile vipande thelathini vya fedha, nikamtupia huyo mfinyanzi ndani ya nyumba ya Bwana.
14. Ndipo nikaikata vipande viwili fimbo yangu ya pili, iitwayo Vifungo, ili nipate kuuvunja udugu uliokuwa kati ya Yuda na Israeli.
15. Bwana akaniambia, Jitwalie tena vyombo vya mchungaji mpumbavu.
16. Kwa maana, tazama, mimi nitainua katika nchi hii mchungaji, ambaye hatawaangalia waliopotea, wala hatawatafuta waliotawanyika, wala hatamganga aliyevunjika, wala hatamlisha aliye mzima; bali atakula nyama ya wanono, na kuzirarua-rarua kwato zao.
17. Ole wake mchungaji asiyefaa, aliachaye kundi! Upanga utakuwa juu ya mkono wake, na juu ya jicho lake la kuume; mkono wake utakuwa umekauka kabisa, na jicho lake la kuume litakuwa limepofuka.

  Zechariah (11/14)