Zechariah (10/14)  

1. Mwombeni Bwana mvua wakati wa masika, naam, Bwana afanyaye umeme, naye atawapa manyunyu ya mvua, kila mtu atapewa nyasi kondeni.
2. Kwa maana vinyago vimenena maneno ya ubatili, nao waaguzi wameona uongo; nao wameleta habari za ndoto za uongo, wafariji bure; kwa sababu hiyo waenda zao kama kondoo, wateswa, kwa sababu hapana mchungaji.
3. Hasira yangu imewaka juu ya wachungaji, nami nitawaadhibu mbuzi waume; kwa maana Bwana wa majeshi ameliangalia kundi lake, yaani, nyumba ya Yuda, naye atawafanya kuwa kama farasi wake mzuri vitani.
4. Kwake yeye litatoka lile jiwe la pembeni, kwake yeye utatoka msumari, kwake yeye utatoka upinde wa vita, kwake yeye atatoka kila mtawala pamoja.
5. Nao watakuwa kama mashujaa, wakanyagao adui zao katika matope ya njia vitani; nao watapiga vita, kwa sababu Bwana yu pamoja nao; na hao wapandao farasi watafadhaishwa.
6. Nami nitaitia nguvu nyumba ya Yuda, nami nitaiokoa nyumba ya Yusufu, nami nitawarudisha, kwa maana nawaonea rehema; nao watakuwa kana kwamba sikuwatupa; kwa maana mimi ni Bwana, Mungu wao, nami nitawasikia.
7. Na watu wa Efraimu watakuwa kama shujaa, na moyo wao utafurahi kana kwamba ni kwa divai; naam, watoto wao wataona mambo haya, na kufurahi; mioyo yao itamfurahia Bwana.
8. Nitawapigia kelele, na kuwakusanya pamoja; kwa maana nimewakomboa; nao wataongezeka kama walivyoongezeka.
9. Nami nitawapanda kama mbegu kati ya mataifa; nao watanikumbuka katika nchi zilizo mbali; nao watakaa pamoja na watoto wao; tena watarudi.
10. Tena nitawarudisha toka nchi ya Misri, nitawakusanya na kuwatoa katika Ashuru; nami nitawaingiza katika nchi ya Gileadi na Lebanoni; ila nafasi ya kuwatosha haitaonekana.
11. Naye atapita kati ya bahari ya mateso, na kuyapiga mawimbi ya bahari, na vilindi vyote vya mto wa Nile vitakauka; na kiburi cha Ashuru kitashushwa; na fimbo ya enzi ya Misri itatoweka.
12. Nami nitawatia nguvu katika Bwana; nao watatembea huko na huko katika jina lake, asema Bwana.

  Zechariah (10/14)