| ← SongOfSongs (7/8) → |
| 1. | Siti msharifu, jinsi zilivyo nzuri Hatua zako katika mitalawanda. Mapaja yako ya mviringo ni kama johari, Kazi ya mikono ya fundi mstadi; |
| 2. | Kitovu chako ni kama bilauri iliyoviringana, Na isikose divai iliyochanganyika; Tumbo lako ni mfano wa chungu ya ngano, Iliyozungukwa na ugo wa nyinyoro; |
| 3. | Maziwa yako mawili ni kama wana-paa wawili, Ambao ni mapacha ya paa; |
| 4. | Shingo yako ni kama huo mnara wa pembe; Macho yako kama viziwa vya Heshboni, Karibu na mlango wa Beth-rabi; Pua yako ni kama mnara wa Lebanoni, Unaoelekea Dameski; |
| 5. | Kichwa chako juu yako ni kama Karmeli, Na nywele za kichwa chako kama urujuani, Mfalme amenaswa na mashungu yake. |
| 6. | Jinsi yalivyo mazuri, yalivyo matamu, Mapenzi katikati ya anasa! |
| 7. | Kimo chako kimefanana na mtende, Na maziwa yako na vichala. |
| 8. | Nilisema, Nitapanda huo mtende, Na kuyashika makuti yake. Maziwa yako na yawe kama vichala vya mzabibu, Na harufu ya pumzi yako kama mapera; |
| 9. | Na kinywa chako kama divai iliyo bora, Kwa mpendwa wangu inashuka taratibu, Ikitiririka midomoni mwao walalao. |
| 10. | Mimi ni wake mpendwa wangu, Na shauku yake ni juu yangu. |
| 11. | Njoo, mpendwa wangu, twende mashambani, Tufanye maskani katika vijiji. |
| 12. | Twende mapema hata mashamba ya mizabibu, Tuone kama mzabihu umechanua, Na maua yake yamefunuka; Kama mikomamanga imetoa maua; Huko nitakupa pambaja zangu. |
| 13. | Mitunguja hutoa harufu yake; Juu ya milango yetu yako matunda mazuri, Mapya na ya kale, ya kila namna, Niliyokuwekea, mpendwa wangu. |
| ← SongOfSongs (7/8) → |