| ← SongOfSongs (6/8) → |
| 1. | Mpendwa wako amekwenda wapi, Wewe uliye mzuri katika wanawake? Mpendwa wako amegeukia upande upi, Ili tumtafute pamoja nawe? |
| 2. | Mpendwa wangu ameshukia bustani yake, Kwenye matuta ya rihani; Ili kulisha penye bustani, Ili kuchuma nyinyoro. |
| 3. | Mimi ni wake mpendwa wangu, naye ni wangu, Hulisha kundi lake penye nyinyoro. |
| 4. | Mpenzi wangu, u mzuri kama Tirza, Mwenye kupendeza kama Yerusalemu, Wa kutisha kama wenye bendera. |
| 5. | Uyageuzie macho yako mbali nami, Kwa maana yamenitisha sana. Nywele zako ni kama kundi la mbuzi, Wakijilaza mbavuni pa Gileadi. |
| 6. | Meno yako kama kundi la kondoo, Wakipanda kutoka kuoshwa; Ambao kila mmoja amezaa mapacha, Wala hakuna aliyefiwa kati yao. |
| 7. | Mashavu yako ni kama kipande cha komamanga, Nyuma ya barakoa yako. |
| 8. | Wako malkia sitini, na masuria themanini, Na wanawali wasiohesabika; |
| 9. | Hua wangu, mkamilifu wangu, ni mmoja tu, Mtoto wa pekee wa mamaye. Ndiye kipenzi chake aliyemzaa, Binti wakamwona wakamwita heri; Malkia na masuria nao wakamwona, Wakamsifu, wakisema, |
| 10. | Ni nani huyu atazamaye kama alfajiri, Mzuri kama mwezi, safi kama jua, Wa kutisha kama wenye bendera? |
| 11. | Nalishukia bustani ya milozi, Ili kuyatazama machipuko ya bondeni; Nione kama mzabibu umechanua, Kama mikomamanga imetoa maua. |
| 12. | Kabla sijajua, roho yangu ilinileta Katikati ya magari ya wakuu wangu. |
| 13. | Rudi, rudi, Mshulami, Rudi, rudi, ili sisi tukutazame. |
| ← SongOfSongs (6/8) → |