| ← SongOfSongs (3/8) → |
| 1. | Usiku kitandani nalimtafuta mpendwa wa nafsi yangu, Nalimtafuta, nisimpate. |
| 2. | Nikasema, Haya, niondoke nizunguke mjini, Katika njia zake na viwanjani, Nimtafute mpendwa wa nafsi yangu. Nikamtafuta, nisimpate. |
| 3. | Walinzi wazungukao mjini waliniona; Je! Mmemwona mpendwa wa nafsi yangu? |
| 4. | Kitambo kidogo tu nikiisha kuwaondokea, Nikamwona mpendwa wa nafsi yangu; Nikamshika, nisimwache tena, Hata nilipomleta nyumbani mwa mamangu, Chumbani mwake aliyenizaa. |
| 5. | Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe. |
| 6. | Ni nani huyu apandaye kutoka nyikani, Mfano wake ni nguzo za moshi; Afukizwa manemane na ubani, Na mavumbi ya manukato yote ya mchuuzi? |
| 7. | Tazama, ni machela yake Sulemani; Mashujaa sitini waizunguka, Wa mashujaa wa Israeli. |
| 8. | Wote wameshika upanga, Wamehitimu kupigana; Kila mtu anao upanga wake pajani Kwa hofu ya kamsa za usiku. |
| 9. | Mfalme Sulemani alijifanyizia machela Ya miti ya Lebanoni; |
| 10. | Nguzo zake alizifanyiza za fedha, Na mgongo wake wa dhahabu, Kiti chake kimepambwa urujuani, Gari lake limenakishiwa njumu, Hiba ya binti za Yerusalemu. |
| 11. | Tokeni, enyi binti za Sayuni, Mtazameni Mfalme Sulemani, Amevaa taji alivyovikwa na mamaye, Siku ya maposo yake, Siku ya furaha ya moyo wake. |
| ← SongOfSongs (3/8) → |