← SongOfSongs (2/8) → |
1. | Mimi ni ua la uwandani, |
2. | Kama nyinyoro kati ya miiba, Kadhalika mpenzi wangu kati ya binti. |
3. | Kama mpera kati ya miti ya msituni, Kadhalika mpendwa wangu kati ya vijana. Naliketi kivulini mwake kwa furaha, Na matunda yake naliyaonja kuwa matamu. |
4. | Akanileta mpaka nyumba ya karamu, Na bendera yake juu yangu ni mapenzi. |
5. | Nishibisheni zabibu, niburudisheni kwa mapera, Kwa maana nimezimia kwa mapenzi. |
6. | Mkono wake wa kushoto uko chini ya kichwa changu, Nao wa kuume unanikumbatia! |
7. | Nawasihi, enyi binti za Yerusalemu, Kwa paa na kwa ayala wa porini, Msiyachochee mapenzi, wala kuyaamsha, Hata yatakapoona vema yenyewe. |
8. | Sikiliza! Ni mpendwa wangu! Tazama, anakuja, Akiruka milimani, akichachawa vilimani. |
9. | Mpendwa wangu ni kama paa, au ayala. Tazama, asimama nyuma ya ukuta wetu, Achungulia dirishani, atazama kimiani. |
10. | Mpendwa wangu alinena, akaniambia, Ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako, |
11. | Maana tazama, kaskazi imepita, Masika imekwisha, imekwenda zake; |
12. | Maua yatokea katika nchi, Wakati wa kupelea umefika, Na sauti ya mwigo husikiwa kwetu. |
13. | Mtini wapevusha tini zake, Na mizabibu inachanua, Inatoa harufu yake nzuri; Ondoka, mpenzi wangu, mzuri wangu, uje zako. |
14. | Hua wangu, mafichoni mwa jabali, Katika sitara za magenge, Nitazame uso wako, nisikie sauti yako, Maana sauti yako ni tamu na uso wako mzuri. |
15. | Tukamatie mbweha, Wale mbweha wadogo, Waiharibuo mizabibu, Maana mizabibu yetu yachanua. |
16. | Mpendwa wangu ni wangu, na mimi ni wake; Hulisha kundi lake penye nyinyoro. |
17. | Hata jua lipunge, na vivuli vikimbie, Unigeukie, mpendwa wangu, Nawe uwe kama paa, au ayala, Juu ya milima ya Betheri. |
← SongOfSongs (2/8) → |