Romans (9/16)  

1. Nasema kweli katika Kristo, sisemi uongo, dhamiri yangu ikinishuhudia katika Roho Mtakatifu,
2. ya kwamba nina huzuni nyingi na maumivu yasiyokoma moyoni mwangu.
3. Kwa maana ningeweza kuomba mimi mwenyewe niharimishwe na kutengwa na Kristo kwa ajili ya ndugu zangu, jamaa zangu kwa jinsi ya mwili;
4. ambao ni Waisraeli, wenye kule kufanywa wana, na ule utukufu, na maagano, na kupewa torati, na ibada ya Mungu, na ahadi zake;
5. ambao mababu ni wao, na katika hao alitoka Kristo kwa jinsi ya mwili. Ndiye aliye juu ya mambo yote, Mungu, mwenye kuhimidiwa milele. Amina.
6. Si kana kwamba neno la Mungu limetanguka. Maana hawawi wote Waisraeli walio wa uzao wa Israeli.
7. Wala hawawi wote wana kwa kuwa wazao wa Ibrahimu, bali, Katika Isaka wazao wako wataitwa;
8. yaani, si watoto wa mwili walio watoto wa Mungu, bali watoto wa ile ahadi wanahesabiwa kuwa wazao.
9. Kwa maana neno la ahadi ni hili, Panapo wakati huu nitakuja, na Sara atakuwa na mwana.
10. Wala si hivyo tu, lakini Rebeka naye, akiisha kuchukua mimba kwa mume mmoja, naye ni Isaka, baba yetu,
11. (kwa maana kabla hawajazaliwa wale watoto, wala hawajatenda neno jema wala baya, ili lisimame kusudi la Mungu la kuchagua, si kwa sababu ya matendo, bali kwa sababu ya nia yake aitaye),
12. aliambiwa hivi, Mkubwa atamtumikia mdogo.
13. Kama ilivyoandikwa, Nimempenda Yakobo, bali Esau nimemchukia.
14. Tuseme nini basi? Kuna udhalimu kwa Mungu? Hasha!
15. Maana amwambia Musa, Nitamrehemu yeye nimrehemuye, nitamhurumia yeye nimhurumiaye.
16. Basi, kama ni hivyo, si katika uwezo wa yule atakaye, wala wa yule apigaye mbio; bali wa yule arehemuye, yaani, Mungu.
17. Kwa maana maandiko yasema juu ya Farao, ya kwamba, Nilikusimamisha kwa kusudi hili, ili nionyeshe nguvu zangu kwako, jina langu likatangazwe katika nchi yote.
18. Basi, kama ni hivyo, atakaye kumrehemu humrehemu, na atakaye kumfanya mgumu humfanya mgumu.
19. Basi, utaniambia, Mbona angali akilaumu? Kwa maana ni nani ashindanaye na kusudi lake?
20. La! Sivyo, Ee binadamu; wewe u nani umjibuye Mungu? Je! Kitu kilichoumbwa kimwambie yeye aliyekiumba, Kwani kuniumba hivi?
21. Au mfinyanzi je! Hana amri juu ya udongo, kwa fungu moja la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima, na kimoja kiwe hakina heshima?
22. Ni nini basi, ikiwa Mungu kwa kutaka kuonyesha ghadhabu yake, na kuudhihirisha uweza wake, kwa uvumilivu mwingi, alichukuliana na vile vyombo vya ghadhabu vilivyofanywa tayari kwa uharibifu;
23. tena, ili audhihirishe wingi wa utukufu wake katika vile vyombo vya rehema, alivyovitengeneza tangu zamani vipate utukufu;
24. ndio sisi aliotuita, si watu wa Wayahudi tu, ila na watu wa Mataifa pia?
25. Ni kama vile alivyosema katika Hosea, Nitawaita watu wangu wale wasiokuwa watu wangu, Na mpenzi wangu yeye asiyekuwa mpenzi wangu.
26. Tena itakuwa mahali pale walipoambiwa, Ninyi si watu wangu, Hapo wataitwa wana wa Mungu aliye hai.
27. Isaya naye atoa sauti yake juu ya Israeli, kusema,
28. Kwa maana Bwana atalitekeleza neno lake juu ya nchi, akilimaliza na kulikata.
29. Tena kama Isaya alivyotangulia kunena,
30. Tuseme nini, basi? Ya kwamba watu wa Mataifa, wasioifuata haki, walipata haki; lakini ni ile haki iliyo ya imani;
31. bali Israeli wakiifuata sheria ya haki hawakuifikilia ile sheria.
32. Kwa sababu gani? Kwa sababu hawakuifuata kwa njia ya imani, bali kana kwamba kwa njia ya matendo. Wakajikwaa juu ya jiwe lile likwazalo,
33. kama ilivyoandikwa,

  Romans (9/16)