Romans (4/16)  

1. Basi, tusemeje juu ya Ibrahimu, baba yetu kwa jinsi ya mwili?
2. Kwa maana ikiwa Ibrahimu alihesabiwa haki kwa ajili ya matendo yake, analo la kujisifia; lakini si mbele za Mungu.
3. Maana maandiko yasemaje? Ibrahimu alimwamini Mungu, ikahesabiwa kwake kuwa haki.
4. Lakini kwa mtu afanyaye kazi, ujira wake hauhesabiwi kuwa ni neema, bali kuwa ni deni.
5. Lakini kwa mtu asiyefanya kazi, bali anamwamini yeye ambaye amhesabia haki asiyekuwa mtauwa, imani yake mtu huyo imehesabiwa kuwa haki.
6. Kama vile Daudi aunenavyo uheri wake mtu yule ambaye Mungu amhesabia kuwa na haki pasipo matendo,
7. Heri waliosamehewa makosa yao, Na waliositiriwa dhambi zao.
8. Heri mtu yule ambaye Bwana hamhesabii dhambi.
9. Basi je! Uheri huo ni kwa hao waliotahiriwa, au kwa hao pia wasiotahiriwa? Kwa kuwa twanena ya kwamba kwake Ibrahimu imani yake ilihesabiwa kuwa ni haki.
10. Alihesabiwaje basi? Alipokwisha kutahiriwa, au kabla hajatahiriwa? Si baada ya kutahiriwa, bali kabla ya kutahiriwa.
11. Naye aliipokea dalili hii ya kutahiriwa, muhuri ya ile haki ya imani aliyokuwa nayo kabla hajatahiriwa; apate kuwa baba yao wote waaminio, ijapokuwa hawakutahiriwa, ili na wao pia wahesabiwe haki;
12. tena awe baba ya kutahiriwa, kwa wale ambao si waliotahiriwa tu, bali pia wanazifuata nyayo za imani yake baba yetu Ibrahimu aliyokuwa nayo kabla hajatahiriwa.
13. Kwa maana ahadi ile ya kwamba atakuwa mrithi wa ulimwengu alipewa Ibrahimu na uzao wake, si kwa sheria bali kwa haki aliyohesabiwa kwa imani.
14. Maana ikiwa wale wa sheria ndio warithi, imani imekuwa bure, na ahadi imebatilika.
15. Kwa sababu sheria ndiyo ifanyayo hasira; maana pasipokuwapo sheria, hapana kosa.
16. Kwa hiyo ilitoka katika imani, iwe kwa njia ya neema, ili kwamba ile ahadi iwe imara kwa wazao wote; si kwa wale wa torati tu, ila na kwa wale wa imani ya Ibrahimu; aliye baba yetu sisi sote;
17. (kama ilivyoandikwa, Nimekuweka kuwa baba wa mataifa mengi); mbele zake yeye aliyemwamini, yaani Mungu, mwenye kuwahuisha wafu, ayatajaye yale yasiyokuwako kana kwamba yamekuwako.
18. Naye aliamini kwa kutarajia yasiyoweza kutarajiwa, ili apate kuwa baba wa mataifa mengi, kama ilivyonenwa, Ndivyo utakavyokuwa uzao wako.
19. Yeye asiyekuwa dhaifu wa imani, alifikiri hali ya mwili wake uliokuwa umekwisha kufa, (akiwa amekwisha kupata umri wa kama miaka mia), na hali ya kufa ya tumbo lake Sara.
20. Lakini akiiona ahadi ya Mungu hakusita kwa kutokuamini, bali alitiwa nguvu kwa imani, akimtukuza Mungu;
21. huku akijua hakika ya kuwa Mungu aweza kufanya yale aliyoahidi.
22. Kwa hiyo ilihesabiwa kwake kuwa ni haki.
23. Walakini haikuandikwa kwa ajili yake tu kwamba ilihesabiwa kwake;
24. bali na kwa ajili yetu sisi mtakaohesabiwa vivyo hivyo, sisi tunaomwamini yeye aliyemfufua Yesu Bwana wetu katika wafu;
25. ambaye alitolewa kwa ajili ya makosa yetu, na kufufuliwa ili mpate kuhesabiwa haki.

  Romans (4/16)