Romans (3/16)  

1. Basi Myahudi ana ziada gani? Na kutahiriwa kwafaa nini?
2. Kwafaa sana kwa kila njia. Kwanza kwa kuwa wamekabidhiwa mausia ya Mungu.
3. Ni nini, basi, ikiwa baadhi yao hawakuamini? Je! Kutokuamini kwao kutaubatili uaminifu wa Mungu?
4. Hasha! Mungu aonekane kuwa amini na kila mtu mwongo; kama ilivyoandikwa, Ili ujulike kuwa una haki katika maneno yako, Ukashinde uingiapo katika hukumu.
5. Lakini, ikiwa udhalimu wetu waithibitisha haki ya Mungu, tuseme nini? Je! Mungu ni dhalimu aletaye ghadhabu? (Nasema kwa jinsi ya kibinadamu.)
6. Hasha! Kwa maana hapo Mungu atawezaje kuuhukumu ulimwengu?
7. Lakini, ikiwa kweli ya Mungu imezidi kudhihirisha utukufu wake kwa sababu ya uongo wangu, mbona mimi ningali nahukumiwa kuwa ni mwenye dhambi?
8. Kwa nini tusiseme (kama tulivyosingiziwa, na kama wengine wanavyokaza kusema ya kwamba twasema hivyo), Na tufanye mabaya, ili yaje mema? Ambao kuhukumiwa kwao kuna haki.
9. Ni nini basi? Tu bora kuliko wengine? La! Hata kidogo. Kwa maana tumekwisha kuwashitaki Wayahudi na Wayunani ya kwamba pia wamekuwa chini ya dhambi;
10. kama ilivyoandikwa, ya kwamba, Hakuna mwenye haki hata mmoja.
11. Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu.
12. Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja.
13. Koo lao ni kaburi wazi, Kwa ndimi zao wametumia hila. Sumu ya fira i chini ya midomo yao.
14. Vinywa vyao vimejaa laana na uchungu.
15. Miguu yao ina mbio kumwaga damu.
16. Uharibifu na mashaka yamo njiani mwao.
17. Wala njia ya amani hawakuijua.
18. Kumcha Mungu hakupo machoni pao.
19. Basi twajua ya kuwa mambo yote inenayo torati huyanena kwa hao walio chini ya torati, ili kila kinywa kifumbwe, na ulimwengu wote uwe chini ya hukumu ya Mungu;
20. kwa sababu hakuna mwenye mwili atakayehesabiwa haki mbele zake kwa matendo ya sheria; kwa maana kutambua dhambi huja kwa njia ya sheria.
21. Lakini sasa, haki ya Mungu imedhihirika pasipo sheria; inashuhudiwa na torati na manabii;
22. ni haki ya Mungu iliyo kwa njia ya imani katika Yesu Kristo kwa wote waaminio. Maana hakuna tofauti;
23. kwa sababu wote wamefanya dhambi, na kupungukiwa na utukufu wa Mungu;
24. wanahesabiwa haki bure kwa neema yake, kwa njia ya ukombozi ulio katika Kristo Yesu;
25. ambaye Mungu amekwisha kumweka awe upatanisho
26. apate kuonyesha haki yake wakati huu, ili awe mwenye haki na mwenye kumhesabu haki yeye amwaminiye Yesu.
27. Ku wapi, basi, kujisifu? Kumefungiwa nje. Kwa sheria ya namna gani? Kwa sheria ya matendo? La! Bali kwa sheria ya imani.
28. Basi, twaona ya kuwa mwanadamu huhesabiwa haki kwa imani pasipo matendo ya sheria.
29. Au je! Mungu ni Mungu wa Wayahudi tu? Siye Mungu wa Mataifa pia? Naam, ni Mungu wa Mataifa pia;
30. kama kwa kweli Mungu ni mmoja, atakayewahesabia haki wale waliotahiriwa katika imani, nao wale wasiotahiriwa atawahesabia haki kwa njia ya imani iyo hiyo.
31. Basi, je! Twaibatilisha sheria kwa imani hiyo? Hasha! Kinyume cha hayo twaithibitisha sheria.

  Romans (3/16)