Romans (12/16)  

1. Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.
2. Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.
3. Kwa maana kwa neema niliyopewa namwambia kila mtu aliyeko kwenu asinie makuu kupita ilivyompasa kunia; bali awe na nia ya kiasi, kama Mungu alivyomgawia kila mtu kiasi cha imani.
4. Kwa kuwa kama vile katika mwili mmoja tuna viungo vingi, wala viungo vyote havitendi kazi moja;
5. Vivyo hivyo na sisi tulio wengi tu mwili mmoja katika Kristo, na viungo, kila mmoja kwa mwenzake.
6. Basi kwa kuwa tuna karama zilizo mbalimbali, kwa kadiri ya neema mliyopewa; ikiwa unabii, tutoe unabii kwa kadiri ya imani;
7. ikiwa huduma, tuwemo katika huduma yetu; mwenye kufundisha, katika kufundisha kwake;
8. mwenye kuonya, katika kuonya kwake; mwenye kukirimu, kwa moyo mweupe; mwenye kusimamia kwa bidii mwenye kurehemu, kwa furaha.
9. Pendo na lisiwe na unafiki lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema.
10. Kwa pendo la udugu, mpendane ninyi kwa ninyi; kwa heshima mkiwatanguliza wenzenu;
11. kwa bidii, si walegevu; mkiwa na juhudi katika roho zenu; mkimtumikia Bwana;
12. kwa tumaini, mkifurahi; katika dhiki, mkisubiri; katika kusali, mkidumu;
13. kwa mahitaji ya watakatifu, mkifuata ukarimu; katika kukaribisha wageni mkijitahidi.
14. Wabarikini wanaowaudhi; barikini, wala msilaani.
15. Furahini pamoja nao wafurahio; lieni pamoja nao waliao.
16. Mpatane nia zenu ninyi kwa ninyi. Msinie yaliyo makuu, lakini mkubali kushughulishwa na mambo manyonge. Msiwe watu wa kujivunia akili.
17. Msimlipe mtu ovu kwa ovu. Angalieni yaliyo mema machoni pa watu wote.
18. Kama yamkini, kwa upande wenu, mkae katika amani na watu wote.
19. Wapenzi, msijilipize kisasi, bali ipisheni ghadhabu ya Mungu; maana imeandikwa, Kisasi ni juu yangu mimi; mimi nitalipa, anena Bwana.
20. Lakini, Adui yako akiwa na njaa, mlishe; akiwa na kiu, mnyweshe; maana ufanyapo hivyo, utampalia makaa ya moto kichwani pake.
21. Usishindwe na ubaya, bali uushinde ubaya kwa wema.

  Romans (12/16)