Revelation (7/22)  

1. Baada ya hayo nikaona malaika wanne wamesimama katika pembe nne za nchi, wakizizuia pepo nne za nchi, upepo usivume juu ya nchi, wala juu ya bahari, wala juu ya mti wo wote.
2. Nikaona malaika mwingine, akipanda kutoka maawio ya jua, mwenye muhuri ya Mungu aliye hai; akawapigia kelele kwa sauti kuu wale malaika wanne waliopewa kuidhuru nchi na bahari,
3. akisema, Msiidhuru nchi, wala bahari, wala miti, hata tutakapokwisha kuwatia muhuri watumwa wa Mungu wetu juu ya vipaji vya nyuso zao.
4. Nikasikia hesabu yao waliotiwa muhuri katika kila kabila ya Waisraeli, watu mia na arobaini na nne elfu.
5. Wa kabila ya Yuda kumi na mbili elfu waliotiwa muhuri. Wa kabila ya Reubeni kumi na mbili elfu. Wa kabila ya Gadi kumi na mbili elfu.
6. Wa kabila ya Asheri kumi na mbili elfu. Wa kabila ya Naftali kumi na mbili elfu. Wa kabila ya Manase kumi na mbili elfu.
7. Wa kabila ya Simeoni kumi na mbili elfu. Wa kabila ya Lawi kumi na mbili elfu. Wa kabila ya Isakari kumi na mbili elfu.
8. Wa kabila ya Zabuloni kumi na mbili elfu. Wa kabila ya Yusufu kumi na mbili elfu. Wa kabila ya Benyamini kumi na mbili elfu waliotiwa muhuri.
9. Baada ya hayo nikaona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti cha enzi, na mbele za Mwana-Kondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi mwao;
10. wakilia kwa sauti kuu wakisema, Wokovu una Mungu wetu aketiye katika kiti cha enzi, na Mwana-Kondoo.
11. Na malaika wote walikuwa wakisimama pande zote za kile kiti cha enzi, na za hao wazee, na za wale wenye uhai wanne, nao wakaanguka kifulifuli mbele ya kile kiti cha enzi, wakamsujudu Mungu,
12. wakisema, Amina; Baraka na utukufu na hekima na shukrani na heshima na uweza na nguvu zina Mungu wetu hata milele na milele. Amina.
13. Akajibu mmoja wa wale wazee akiniambia, Je! Watu hawa waliovikwa mavazi meupe ni akina nani? Na wametoka wapi?
14. Nikamwambia, Bwana wangu, wajua wewe. Akaniambia, Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwana-Kondoo.
15. Kwa hiyo wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu, nao wanamtumikia mchana na usiku katika hekalu lake, na yeye aketiye katika kiti cha enzi atatanda hema yake juu yao.
16. Hawataona njaa tena, wala hawataona kiu tena, wala jua halitawapiga, wala hari iliyo yote.
17. Kwa maana huyo Mwana-Kondoo, aliye katikati ya kiti cha enzi, atawachunga, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji yenye uhai, na Mungu atayafuta machozi yote katika macho yao.

  Revelation (7/22)