| ← Revelation (16/22) → | 
| 1. | Nikasikia sauti kuu kutoka hekaluni, ikiwaambia wale malaika saba, Enendeni, mkavimimine vile vitasa saba vya ghadhabu ya Mungu juu ya nchi. | 
| 2. | Akaenda huyo wa kwanza, akakimimina kitasa chake juu ya nchi; pakawa na jipu baya, bovu, juu ya wale watu wenye chapa ya huyo mnyama, na wale wenye kuisujudia sanamu yake. | 
| 3. | Na huyo wa pili akakimimina kitasa chake juu ya bahari, ikawa damu kama damu ya mfu, na vitu vyote vyenye roho ya uhai katika bahari vikafa. | 
| 4. | Na huyo wa tatu akakimimina kitasa chake juu ya mito na chemchemi za maji; zikawa damu. | 
| 5. | Nami nikamsikia malaika wa maji akisema, Wewe u mwenye haki, uliyeko na uliyekuwako, Mtakatifu, kwa kuwa umehukumu hivi; | 
| 6. | kwa kuwa walimwaga damu ya watakatifu na ya manabii, nawe umewapa damu wainywe; nao wamestahili. | 
| 7. | Nikaisikia hiyo madhabahu ikisema, Naam, Bwana Mungu Mwenyezi, ni za kweli, na za haki, hukumu zako. | 
| 8. | Na huyo wa nne akakimimina kitasa chake juu ya jua, nalo likapewa kuwaunguza wanadamu kwa moto. | 
| 9. | Wanadamu wakaunguzwa maunguzo makubwa, nao wakalitukana jina la Mungu aliye na mamlaka juu ya mapigo hayo; wala hawakutubu wala kumpa utukufu. | 
| 10. | Na huyo wa tano akakimimina kitasa chake juu ya kiti cha enzi cha yule mnyama; ufalme wake ukatiwa giza; wakatafuna ndimi zao kwa sababu ya maumivu, | 
| 11. | wakamtukana Mungu wa mbingu kwa sababu ya maumivu yao, na kwa sababu ya majipu yao; wala hawakuyatubia matendo yao. | 
| 12. | Na huyo wa sita akakimimina kitasa chake juu ya mto ule mkubwa Frati; maji yake yakakauka, ili njia itengenezwe kwa wafalme watokao katika maawio ya jua. | 
| 13. | Nikaona roho tatu za uchafu zilizofanana na vyura, zikitoka katika kinywa cha yule joka, na katika kinywa cha yule mnyama, na katika kinywa cha yule nabii wa uongo. | 
| 14. | Hizo ndizo roho za mashetani, zifanyazo ishara, zitokazo na kuwaendea wafalme wa ulimwengu wote kuwakusanya kwa vita ya siku ile kuu ya Mungu Mwenyezi. | 
| 15. | (Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.) | 
| 16. | Wakawakusanya hata mahali paitwapo kwa Kiebrania, Har-Magedoni. | 
| 17. | Na huyo wa saba akakimimina kitasa chake juu ya anga. Sauti kuu ikatoka katika hekalu, katika kile kiti cha enzi, ikisema, Imekwisha kuwa. | 
| 18. | Pakawa na umeme na sauti na radi; na palikuwa na tetemeko la nchi kubwa, ambalo tangu wanadamu kuwako juu ya nchi hapakuwa namna ile, jinsi lilivyokuwa kubwa tetemeko hilo. | 
| 19. | Na mji ule mkuu ukagawanyikana mafungu matatu, na miji ya mataifa ikaanguka; na Babeli ule mkuu ukakumbukwa mbele za Mungu, kupewa kikombe cha mvinyo ya ghadhabu ya hasira yake. | 
| 20. | Kila kisiwa kikakimbia, wala milima haikuonekana tena. | 
| 21. | Na mvua ya mawe kubwa sana, ya mawe mazito kama talanta, ikashuka kutoka mbinguni juu ya wanadamu. Wanadamu wakamtukana Mungu kwa sababu ya lile pigo la mvua ya mawe; kwa maana pigo lake ni kubwa mno. | 
| ← Revelation (16/22) → |