| ← Psalms (97/150) → |
| 1. | Bwana ametamalaki, nchi na ishangilie, Visiwa vingi na vifurahi. |
| 2. | Mawingu na giza vyamzunguka, Haki na hukumu ndio msingi wa kiti chake. |
| 3. | Moto hutangulia mbele zake, Nao huwateketeza watesi wake pande zote. |
| 4. | Umeme wake uliuangaza ulimwengu, Nchi ikaona ikatetemeka. |
| 5. | Milima iliyeyuka kama nta mbele za Bwana, Mbele za Bwana wa dunia yote. |
| 6. | Mbingu zimetangaza haki yake, Na watu wote wameuona utukufu wake. |
| 7. | Na waaibishwe wote waabuduo sanamu, Wajivunao kwa vitu visivyofaa; Enyi miungu yote, msujuduni Yeye. |
| 8. | Sayuni imesikia na kufurahi, Binti za Yuda walishangilia, Kwa sababu ya hukumu zako, Ee Bwana. |
| 9. | Maana Wewe, Bwana, ndiwe Uliye juu, Juu sana kuliko nchi yote; Umetukuka sana juu ya miungu yote. |
| 10. | Enyi mmpendao Bwana, uchukieni uovu; Huwalinda nafsi zao watauwa wake, Na kuwaokoa na mkono wa wasio haki. |
| 11. | Nuru imemzukia mwenye haki, Na furaha wanyofu wa moyo. |
| 12. | Enyi wenye haki, mmfurahieni Bwana, Na kulishukuru jina lake takatifu. |
| ← Psalms (97/150) → |