Psalms (96/150)  

1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya, Mwimbieni Bwana, nchi yote.
2. Mwimbieni Bwana, libarikini jina lake, Tangazeni wokovu wake siku kwa siku.
3. Wahubirini mataifa habari za utukufu wake, Na watu wote habari za maajabu yake.
4. Kwa kuwa Bwana ni mkuu mwenye kusifiwa sana. Na wa kuhofiwa kuliko miungu yote.
5. Maana miungu yote ya watu si kitu, Lakini Bwana ndiye aliyezifanya mbingu.
6. Heshima na adhama ziko mbele zake, Nguvu na uzuri zimo katika patakatifu pake.
7. Mpeni Bwana, enyi jamaa za watu, Mpeni Bwana utukufu na nguvu.
8. Mpeni Bwana utukufu wa jina lake, Leteni sadaka mkaziingie nyua zake.
9. Mwabuduni Bwana kwa uzuri wa utakatifu, Tetemekeni mbele zake, nchi yote.
10. Semeni katika mataifa, Bwana ametamalaki; Naam, ulimwengu umethibitika usitikisike, Atawahukumu watu kwa adili.
11. Mbingu na zifurahi, nchi na ishangilie, Bahari na ivume na vyote viijazavyo,
12. Mashamba na yashangilie, na vyote vilivyomo, Ndipo miti yote ya mwituni iimbe kwa furaha;
13. Mbele za Bwana, kwa maana anakuja, Kwa maana anakuja aihukumu nchi. Atauhukumu ulimwengu kwa haki, Na mataifa kwa uaminifu wake.

  Psalms (96/150)