← Psalms (94/150) → |
1. | Ee Bwana, Mungu wa kisasi, Mungu wa kisasi, uangaze, |
2. | Mwenye kuihukumu nchi, ujitukuze, Uwape wenye kiburi stahili zao. |
3. | Bwana, hata lini wasio haki, Hata lini wasio haki watashangilia? |
4. | Je! Wote watendao uovu watatoa maneno, Na kusema majivuno, na kufanya kiburi? |
5. | Ee Bwana, wanawaseta watu wako; Wanautesa urithi wako; |
6. | Wanamwua mjane na mgeni; Wanawafisha yatima. |
7. | Nao husema, Bwana haoni; Mungu wa Yakobo hafikiri. |
8. | Enyi wajinga miongoni mwa watu, fikirini; Enyi wapumbavu, lini mtakapopata akili? |
9. | Aliyelitia sikio mahali pake asisikie? Aliyelifanya jicho asione? |
10. | Awaadibuye mataifa asikemee? Amfundishaye mwanadamu asijue? |
11. | Bwana anajua mawazo ya mwanadamu, Ya kuwa ni ubatili. |
12. | Ee Bwana, heri mtu yule umwadibuye, Na kumfundisha kwa sheria yako; |
13. | Upate kumstarehesha siku za mabaya, Hata asiye haki atakapochimbiwa shimo. |
14. | Kwa kuwa Bwana hatawatupa watu wake, Wala hutauacha urithi wake, |
15. | Maana hukumu itairejea haki, Na wote walio wanyofu wa moyo wataifuata. |
16. | Ni nani atakayesimama Kwa ajili yangu juu ya wabaya? Ni nani atakayenisaidia Juu yao wafanyao maovu? |
17. | Kama Bwana asingalikuwa msaada wangu, Nafsi yangu kwa upesi ingalikaa penye kimya. |
18. | Niliposema, Mguu wangu unateleza; Ee Bwana, fadhili zako zilinitegemeza. |
19. | Katika wingi wa mawazo ya moyoni mwangu, Faraja zako zaifurahisha roho yangu. |
20. | Je! Kiti cha udhalimu kishirikiane nawe, Kitungacho madhara kwa njia ya sheria? |
21. | Huishambulia nafsi yake mwenye haki, Na kuihukumu damu isiyo na hatia. |
22. | Lakini Bwana amekuwa ngome kwangu, Na Mungu wangu mwamba wangu wa kukimbilia. |
23. | Naye atawarudishia uovu wao, Atawaangamiza katika ubaya wao, Naam, Bwana, Mungu wetu, atawaangamiza. |
← Psalms (94/150) → |