| ← Psalms (91/150) → |
| 1. | Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi. |
| 2. | Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu, Mungu wangu nitakayemtumaini. |
| 3. | Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji, Na katika tauni iharibuyo. |
| 4. | Kwa manyoya yake atakufunika, Chini ya mbawa zake utapata kimbilio; Uaminifu wake ni ngao na kigao. |
| 5. | Hutaogopa hofu ya usiku, Wala mshale urukao mchana, |
| 6. | Wala tauni ipitayo gizani, Wala uele uharibuo adhuhuri, |
| 7. | Ijapo watu elfu waanguka ubavuni pako. Naam, kumi elfu mkono wako wa kuume! Hata hivyo hautakukaribia wewe. |
| 8. | Ila kwa macho yako utatazama, Na kuyaona malipo ya wasio haki. |
| 9. | Kwa kuwa Wewe Bwana ndiwe kimbilio langu; Umemfanya Aliye juu kuwa makao yako. |
| 10. | Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako. |
| 11. | Kwa kuwa atakuagizia malaika zake Wakulinde katika njia zako zote. |
| 12. | Mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe. |
| 13. | Utawakanyaga simba na nyoka, Mwana-simba na joka utawaseta kwa miguu. |
| 14. | Kwa kuwa amekaza kunipenda Nitamwokoa; na kumweka palipo juu, Kwa kuwa amenijua Jina langu. |
| 15. | Ataniita nami nitamwitikia; Nitakuwa pamoja naye taabuni, Nitamwokoa na kumtukuza; |
| 16. | Kwa siku nyingi nitamshibisha, Nami nitamwonyesha wokovu wangu. |
| ← Psalms (91/150) → |